Kaimu Meneja TANROADS Mkoani Rukwa Mhandisi Jetrovas Ngowi akiangalia moja ya sehemu ya barabara kwenye eneo korofi inaloendelewa kujengwa wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Bonde la Ziwa Rukwa
Daraja linalotenga Kijiji cha Mtowisa na kijiji cha Lwanji likiwa limekatika na kusababisha Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalam kushindwa kuendelea na ziara ya ukaguzi wa barabara ya bonde la Ziwa Rukwa.
Kikosi cha Askari waliokuwa katika msafara wa Mkuu wa Mkoa katika Ziara ya ukaguzi wa barabara ya Bonde la Ziwa Rukwa wakisaidia kukwamua moja ya lori la mizigo lililokuwa limekwama muda mfupi baada ya Mkuu wa Mkoa huyo kuahirisha ziara yake.
Kamimu Meneja TANROADS Mkoa wa Rukwa Mhandisi Jetrovas Ngowi (kulia) akitoa maelezo kwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakati wa ziara ya ukaguzi wa Barabara ya Ntendo – Muze inayotoka Manispaa ya Sumbawanga kuelekea katika bonde la Ziwa Rukwa.
********************************************
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Rukwa kuhakikisha wanaharakisha taratibu za malipo ya fedha za wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa madaraja pamoja na makaravati katika barabara ya kilomita 175 inayounganisha mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe katika Bonde la Ziwa Rukwa ili kuwarahisishia wakandarasi hao kufanya kazi kwa wakati na hatimae kurahisha shughuli za kiuchumi za wananchi wa bonde hilo.
Mh. Wangabo ameyasema hayo baada ya kuahirisha ziara yake ya ukaguzi wa barabara hiyo baada ya daraja lililopo katika Kijiji cha Lwanji kukatika usiku wa kuamkia ziara hiyo na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya wananchi wa mikoa hiyo mitatu wanaosafiri kupitia bonde hilo wakati wakandarasi waliopewa kazi za ujenzi na ukarabati wa madaraja hayo wakitumia fedha zao kutekeleza kazi hizo huku TANROAD ikiwa na fedha za kuwalipa ila kuchelewa kutokana na taratibu zao.
“Kuna suala hili la fedha najua fedha zipo kwa Meneja TANROADS, lakini fedha zile hazitoki kwasababu kuna michakato ya kifedha ambayo haijakamilika sasa hatuwezi kwenda namna hii wakati mvua zinanyesha mkandarasi yuko ‘site’ hela hana mpaka 80% hajalipwa na hela iko ofisini, sasa hii hali haikubaliki, wakakamilishe yale masuala ya kimchakato wa fedha ili hawa wakandarasi nao waweze kupata malipo kwasababu wana watu ambao ni vibarua wanapaswa kulipwa kwa kila siku lakini sasa malipo hakuna kwahiyo niwaombe TANROADS wakamilishe michakato yao ya fedha ili fedha ipatikane kwa wakandarasi tuliokoe hili bonde la ziwa Rukwa,” Alisisitiza.
Amesema kuwa ubovu wa barabara hiyo unaathiri shughuli za kiuchumi na za kiafya wananchi wa bonde hilo kiasi cha watu kushindwa kufuata huduma muhimu wanazohitaji kutokana na kukatika kwa ama kufurika kwa mito mingi katika bonde hilo.
Aidha ametwatahadharisha wakandarasi ambao hawana uwezo wa kutekeleza kazi wanazopatiwa huku akiwataka TANROADS kuwachuja wakandarasi hao kabla ya kuwapa kazi hizo kwani huishia kuharibu miundombinu ya barabara na hatimae kuipa hasara serikali kukarabati uharibifu uliofanywa na wakandarasi hao.
“Meneja wa TANROADS ni lazima upitie upya hawa wakandarasi wale wasio na uwezo weka pembeni, wale ambao wana uwezo ndio waendelee na kazi, lakini kwasababu hali ya barabara Pamoja na madaraja ni mbaya sana ninamwagiza Meneja wa TANROADS pamoja na wahandisi wake wote waweke kambi huku Bonde la Ziwa Rukwa mpaka ujenzi huu ukamilike kwasababu hali ni mbaya na usimamizi sio wa karibu sana,” Alisema.
Wakati akiongea mbele ya Waandishi wa Habari Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Jetrovas Ngowi alisema kuwa changamoto kubwa ya barabara hiyo kuharibika kila mara ni kutokana na mito inayotoka milima ya safu ya Lyamba Lyamfipa kuhama njia hali inayosababishwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wananchi wa bonde hilo na kuongeza kuwa tayari wamemshampata mhandisi mshauri anayefanya usanifu yakinifu na wa kina wa barabara hiyo ili kuiepusha serikali kupoteza Zaidi ya Shilingi bilioni 4.4 kila mwaka kufanya ukarabati.
“Shida kubwa ni kwamba mito inahama, unajenga boksi kalavati hapa maji yanahamia kwengine hapa sio kwamba yamejaa ni kutokana na udongo wa huku ni tifutifu kwahiyo maji yanakata sehemu yoyote yanapita, kuna wafugaji wengi kuna wakulima wengi kwa mfano wakulima wa mpunga ndio imekuwa tatizo, tunanya ukarabati kwa gharama ya shilingi bilioni 4.4 kwa mwaka lakini bahati nzuri barabara hii ina mhandisi mshauri anayefanya usanifu yakinifu na wa kina hivyo tunaamini michoro itakayopatikana itamaliza tatizo,” alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliokwama katika eneo hilo akiwemo Bendo Sumuni mkazi wa Kijiji cha Mtowisa amesema kuwa kipindi hiki cha mvua ambapo madaraja mengi huaribika huwa wanaathirika sana hasa kipindi ambacho wanakuwa na shida ya kufuata huduma za afya.
“Kwahiyo tunachoomba katika Kijiji chetu hiki, tunaomba ushirikiano kutoka ngazi za juu waweze kutupatia msaada, kwasababu shida tunazozipata hap ani hatari kwa mfano kuna magari yanayotoka huko mjini yana abiria yakifika hapa watu wanapata shida kwa kuvukia hakupo, na zinazotoka huko ilemba wanakuja hapa hakuna kwa kuvukia, tunaomba mtusaidie,” Alisema.
Barabara hiyo ya Bonde la Ziwa Rukwa iliyoanzia Kijiji cha Kasansa hadi Kijiji cha kilyamatundu ina urefu wa kilometa 175 huku ikiwa na wakandarasi 19 wanaoendelea na ukarabati wa aina mbalimbali ikiwemo madaraja na sehemu korofi ambapo jumla ya Shilingi 4,434,399,500/= zimetengwa kwaajili ya shughuli hizo zinazotegewa kumalizika mwezi Aprili mwaka huu huku wengi wa wakandarasi hao wakiwa wamefikia hatua mbalimbali na wengine kushindwa kuanza ujenzi huo kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha kutekeleza kazi hizo.