Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori Tanzania TAWA, Meja Jenerali Msitaafu, Hamis Semfuko akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi la uzinduzi wa bucha ya kwanza kuuza nyamapori hapa nchini, bucha hilo limefunguliwa Jijini Dodoma.
Kaimu Kamishna wa uhifadhi kutoka Mamlaka ya usimamizi wanyamapori Tanzania TAWA Mabula Misungwi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi la uzinduzi wa bucha ya kwanza kuuza nyamapori hapa nchini, bucha hilo limefunguliwa Jijini Dodoma.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa bucha la kwanza kuuza nyama ya wanyamapori hapa nchini bucha lililofunguliwa jijini Dodoma.
………………………………………………………………….
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori hapa nchini TAWA imeanza rasmi ufunguzi wa mabucha ya nyama yatakayokuwa yakiuza nyama ya wanyamapori hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kufungua bucha ya kwanza ya kuuza nyama hiyo Jijini Dodoma Mwenyekiti wa bodi ya TAWA Meja Jenerali Msitaafu Hamis Semfuko amesema hatua hiyo ni kutimiza maagizo yaliyotolewa na Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa wananchi waanze kunufaika na nyamapori.
“Nimekuja hapa na wajumbe wenzangu kwenye ufunguzi wa bucha la kwanza hapa nchini kuuza nyamapori na hili ni agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa tuhakikishe wananchi wananufaika na rasilimali zao ikiwamo hizi nyamapori” amesema Meja Jenerali Msitaafu Semfuko.
Amesema nyama zitakazopatikana katika mabucha yatakayopata vibali ni kibali maalumu cha uwindaji, windaji wa kitalii, na kwa njia ya hawa wanyamapori watakaokuwa wakifugwa na wananchi kwa vibali maalumu.
“Hizi nyamapori zitatokana na vibali maalumu vya uwindaji, na uwindaji wa kitalii ambapo watalii wanataka nyara kama vichwa wakichukua vichwa nyama zinazobaki ndizo zitapelekwa katika mabucha hayo” amesema.
Amesema kuanzia sasa wananchi watapata vibali vya kufuga wanyamapori ambapo TAWA itawauzia mitamba na wao watakwenda kufuga katika mashamba yao na hii itakwenda kuongeza upatikanaji wa nyamapori katika mabucha hayo na kubainisha kuwa utaratibu huo ndio hutumika Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe.
Amesema sio kwamba kufunguliwa kwa maduka hayo kutaongeza ujangili amebainisha kuwa watadhibiti kikamilifu kuhakikisha nyamapori inayouzwa ni ile iliyopatikana kihalali tu na si kwa njia ya ujangili.
Amewataka wale wote watakao pata vibali vya kuuza nyama hiyo kuzingatia suala la usafi katika mabucha yao ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu, huku akibainisha wanaotaka kufungua mabucha kwenda kuomba vibali TAWA.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa uhifadhi kutoka Mamlaka ya usimamizi wanyamapori Tanzania TAWA Mabula Misungwi amesema TAWA ndio wasimamizi wakuu wa maswala yote yanayohusu uwindaji wa wanyamapori.
Na kubainisha kuwa wao wataendelea kusimamia kikamilifu wanyama pori huku ikiwataka wale wote wanaohitaji kuanzisha biashara hiyo kuwasiliana na Mamlaka hiyo ili wafanye biashara kihalali.