Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uangalizi katika Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa
Jamii, Aloyce Musika, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu
ya idara jijini Dodoma jana. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Taifa ya Huduma kwa Jamii, Jaji Zephrine Galeba.
*************************************
Na Veronica Mwafisi-MOHA-Dodoma
SERIKALI imefanikiwa kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani kupitia
Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291, Sheria ya Majaribio na Ujenzi
wa TabiaSura ya 247 na Sheria ya Magereza Sura ya 34/1967, Kifungu cha
52.
Kwa mujibu wa sheria hizo, wahalifu waliohukumiwa vifungo visivyozidi
miaka mitatu hutumikia adhabu nje ya magereza.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uangalizi katika Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi ambaye Katibu wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii,
Aloyce Musika aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa majukumu ya idara hiyo.
Taarifa hiyo iliwasilishwa kwenye kikao cha kamati ya idara hiyo
kilichofanyika mwishoni mwa wiki Ukumbi wa Mikutano wa TANAPA, Jengo
la Kambarage, jijini Dodoma.
“Lengo la kuanzishwa idara hii ni kuipunguzia serikali gharama za
kuhudumia wafungwa magerezani, kudhibiti tatizo la urudiwaji uhalifu,
kupunguzwa msongamano wa wafungwa magerezani.
“Hadi kufikia Novemba 30, 2020, wafungwa 1,781 walikuwa wanaendelea
kutumikia adhabu za nje ya gereza, wafungwa 1,447 walimaliza kutumikia
adhabu zao,” alisema Musika.
Alifafanua kuwa, mafanikio mengine yaliyofikiwa na kamati hiyo ni
kudumisha amani na utulivu katika jamii, kuimarika mahusiano kati ya
idaara na wadau ambapo hivi sasa idara inafanya kazi kwa karibu na
wadau wote wa haki jinai.
Mafanikio mengine ni kupanua wigo wa kutekeleza majukumu ya idara
katika mikoa yote Tanzania Bara, kununua vitendea kazi, kuipunguzia
serikali ghaarama za kuendesha magereza.
“Dira yetu ni kuwa chombo kinachozingatia weledi, taratibu, vigezo vya
kitaifa na kimataifa katika urekebishaji wahalifu ndani ya jamii,”
alifaafanua Musika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii,
Jaji Zephrine Galeba aliitaka kamati hiyo iendelee kupunguza
msongamano wa wafungwa magerezani.
“Umefika wakati wa kamati kujitathmini kama inaenda mbele au inarudi
nyuma, naomba msirudi nyuma wala kujipangia kiwango kikubwa ili
mtekeleze majukumu yenu,” alisema.
Alimuomba Musika amfikishie salamu za shukrani kutoka kwenye kamati
kwenda kwa Maafisa Huduma kwa Jamii kutokana na utendazi mzuri wa
kazi, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Aliwataka Maafisa Huduma kwa Jamii waendelee kufanya kazi kwa weledi
wakitambua kuwa wamepewa majukumu makubwa hivyo wana mamlaka ambayo si
madogo.
Pia aliwataka wawe na maadili, waaminifu, kuwashukuru wageni wote
waalikwa na baadhi ya Wakuu wa Idara kutoka wizarani kwa kushiriki
kikao hicho.