Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Katavi kama walivyokutwa na mpiga picha wetu katika kibanda cha kuangalia video maeneo ya Mpanda Hotel katika Manispaa ya Mpanda
Na Zillipa Joseph, Katavi
Askofu Mkuu wa Kanisa Kuu Anglikana Dayosisi ya Ziwa Rukwa Mathayo Kasagara ameipongeza jamii kwa kuwa makini na kufuata ushauri wa wataalamu wa Afya katika kipindi chote ambacho Taifa lilikuwa tahadhari juu ya maambukizi ya virusi vya COVID 19
Askofu Kasagara ametoa pongezi hizo wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi mapema leo
‘Kimsingi sisi kama viongozi wa dini tulichukua tahadhari kwa kuweka vyombo vya kusafisha miko na sabuni na tuliwasisitiza waumini kuwa makini na wale wenye watoto wadogo kutokuwaleta watoto kanisani ili kuwaepusha na misongamano’ alisema
‘Pia tulichukua jukumu la kushona barakoa kwa ajili ya waumini wetu na ni jambo la kumshukuru Mungu kwani hakuna hata muumini mmoja aliyepata maambukizi ya COVID 19’ aliongeza
Akizungumzia suala hilo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera amewasifu wakazi wa Katavi kwa kuzingatia ushauri na pia kutumia dawa za asili katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19
‘Hapa watu walijipiga nyungu si mchezo, malimao yalinywewa na kila kaya’ alisema Homera
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha watoto wanafahamu taratibu mila na desturi zao ni wajibu wa jamii kutunza vile vitu vya urithi vilivyoachwa na mababu zetu
Amesema mkoa una mpango wa kujenga kliniki kubwa ya dawa za mitishamba ambayo itatumiwa na watu wa tiba asili na tiba mbadala
‘Tumeshatenga eneo katika viwanja vya nane nane vilivyopo Kabungu wilaya ya Tanganyika na ujenzi utaanza hivi karibuni kwani tayari tuna fedha ya kuanza ujenzi’ alisema Homera
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk. Omar Sukari amesema mkoa wa Katavi ni kati ya mikoa miwili ya Tanzania bara ambayo haikupata wagonjwa wa virusi vya COVID 19
Aidha amewataka wananchi kuendelea kunawa mikono na sabuni kwa kutumia maji tiririka ili kuendelea kujikinga
Dk. Sukari amekiri kuwa hata yeye na familia yake walichukua tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa na kujifukiza
Nao wakazi wa mkoa wa Katavi wamesema wamevuka salama katika kipindi ambacho taifa lilikuwa na tahadhari ya hali ya juu kuhusu korona kwa kuomba na kuvaa barakoa
‘Mimi mke wangu alishona barakoa za vitambaa tukawa tukivaa na watoto’ alisema Hussein Ally mkazi wa Tambuka Reli katika Manispaa ya Mpanda