********************************
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imefanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi milioni 45.760 alizolipwa Mkandarasi wa kampuni ya Leostart Engineering ya jijini Dar es salaam ambapo alilipwa kinyume na utaratibu wa utekelezaji wa mradi wa maji wa kijiji cha Mlongila wilayani Chemba Mkoani humo.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Mkuu taasisi hiyo Bwana Sostenes Kibwengo amesema fedha hizo ni sehemu tu ya fedha alizokuwa amelipwa mkandarasi huyo.
“Mtakumbuka siku za nyuma tuliwahi kuwataarifu kuhusu ufuatiliaji wetu wa mradi huo na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ulionyesha kuwa Mkandarasi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 579.323 ulioanza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2014 alilipwa fedha zaidi ya kazi zilizofanyika na hivyo kutakiwa kuzirejesha.” amesema Kibwengo.
Aidha amebainisha kuwa TAKUKURU imefanikiwa kuwarejeshea zaidi ya shilingi milioni 18 zikiwemo shilingi milioni 9.7 za mfanyabiashara Dismas Kweka mkazi wa Nkuhungu mkoani hapo na shilingi milioni 8.6 za Grace Matona Muuguzi mstaafu na mkazi wa jijini humo.
Amesema Kweka aliuziwa kiwanja Namba 18 kitalu B kilichopo Mbwanga kinyume na utaratibu kwani kiwanja hicho kilitolewa na mwananchi mmoja kama sadaka kwa Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA).
Fedha hizo zimerejeshwa kutoka kwa Richard Mwambeje ambaye alikuwa Katibu wa UWATA alipokea shilingi milioni 19 baada ya kutengeneza mkataba wa kughushi na hivyo kutakiwa kurejesha fedha hizo.
“Huyu jamaa bado anatakiwa kurejesha fedha zilizosalia huku hatua nyingine za kiuchunguzi zikiendelea dhidi ya huyo mtu” amesema.
Kwa upande wa fedha za Muuguzi mstaafu amesema ufuatiliaji wa TAKUKURU umeonyesha kuwa mstaafu huyo aliipatia kampuni ya JW Micro Credit ya jijini hapo toka mwaka 2016 shilingi milioni 20 kwa ahadi ya kulipwa fedha hizo na faida lakini hakulipwa faida wala fedha zake mpaka zinaokolewa.
Pia bwana Kibwengo amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na Halmashauri ya jiji la Dodoma wameweza kuwasaidia wananchi watano kupata viwanja vyao ambavyo walidhulumiwa au walipatiwa eneo ambalo tayari lilikuwa na mmiliki mwingine.
Mkuu huyo wa TAKUKURU ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanaohitaji viwanja kujiridhisha katika maeneo wanayohitaji kabla ya kulipa fedha yoyote.
“Hivi sasa Dodoma kuna matapeli wengi hasa katika eneo la viwanja,mtu asilipe pesa yoyote kabla ya kwenda mamlaka husika kujiridhisha kuhusu umiliki wa kiwanja husika.” amesema.
Katika hatua nyingine mahakama ya wilaya ya Kondoa imemuhukumu mtendaji wa Kata ya Thawi Hashim Ally Mohamed kulipa faini ya shilingi 300,000 au kifungo cha miaka miwili baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi kwamba alishawishi rushwa ya shilingi 175,000 na kupokea shilingi 80,000 ili asimchukulie hatua mzazi ambaye hakumpeleka binti yake sekondari baada ya kufaulu.
Pia mahakama ya hakimu mkazi ya Dodoma imemuhukumu Abdulhakim Kabuga aliyekuwa BVR Operator wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (Nida) kulipa faini ya shilingi 500,000 au kifungo cha miaka mitatu kwa kupokea hongo ya shilingi 30,000 ili amsaidie mtoa taarifa kupata kitambulisho cha uraia mapema.