********************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge Leo amefungua kikao Cha kujadili na kutoa mapendekezo ya namna Bora ya uendeshaji wa mfumo wa kuzuia na kudhibiti uhalifu kwa vyombo vya Moto hususani Bodaboda na Bajaji kwa njia ya mtandao na kuwaelekeza Washiriki kuhakikisha wanafanya uchambuzi wa kina na kutoka na mapendekezo yenye tija.
RC Kunenge amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanazuia uhalifu na kuwawezesha vijana waliojiajiri Katika Bodaboda na Bajaji wanafanya shughuli zao pasipo usumbufu wowote.
Aidha RC Kunenge amesema Mradi huo pia ni muhimu kwakuwa utasaidia Serikali kupata Mapato hivyo ametoa wito kwa washiriki kuchukulia kwa uzito kikao hicho na kutoka na mwongozo mzuri.
Pamoja na hayo RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Kampuni ya TAMOBA Security Force Limited Bw. Joseph Kimisha kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kwa mfumo huo ili wakati utakaoanza kufanya kazi pawepo na ufanisi mkubwa.
Kikao hicho kimehusisha Wadau mbalimbali wakiwemo Kampuni ya TAMOBA Security Limited ambao ndio waratibu, Jeshi la Polisi, Taasisi za Bima, Kampuni za uuzaji wa pikipiki na Bajaji na Wadau wengine wanaohusika na sekta ya Bodaboda na Bajaji.