Msaidizi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Analis Komba kulia,akimsaidia kuvaa joho Mwenyekiti mpya wa Halmashauri hiyo Desdeliu Haule kushoto kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza jipya la madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa mikutano shule ya sekondari Kigonsera wilayani humo, anayeshuhudia katikati makamu mwenyekiti Bahati Kumbele.
…………………………………………
Na Muhidin Amri, Mbinga
KATIBU tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Gilbert Simya,amewataka wataalamu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kutumia elimu yao,kutafuta na kubuni kubuni vyanzo vipya vya mapato vitakavyoisaidia halmashauri hiyo kutekeleza mipango yake ya maendeleo badala ya kusubiri ruzuku kutoka serikali kuu.
Mhandisi Simya amesema hayo mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika kwa zoezi la kuwaapisha madiwani wapya wa halmashauri hiyo lililokwenda sambamba na uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti.
Alisema, uwepo wa vyanzo vingi vya mapato kimsingi vitasaidia sana kuongeza makusanyo na hivyo kukuza mapato yake ya ndani, ambapo halmashauri itaweza kujitegemea na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kuimarika kwa huduma za kijamii.
Kwa mujibu wake,kuna baadhi ya miradi ya maendeleo inayoanzishwa lakini kutokana na ukosefu wa fedha inashindwa kukamilika kwa wakati,kwa kuwa inasubiri fedha kutoka serikali kuu, lakini iwapo halmashauri itakuwa na mapato ya kutosha miradi hiyo itakamilika na kuleta tija kwa wananchi.
Alisema, serikali kuu ina wajibu wa kuisimamia halmashauri katika suala zima la kukusanya mapato yake ya ndani na wao kama viongozi watahakikisha wanakuwa wakali na hata kuwachukulia hatua watumishi watakao shindwa kukusanya na kusimamia kwa namna yoyote mapato yanayopatikana.
Pia Simya ameagiza viongozi wa halmshauri hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi watakaobainika kukusanya mapato ya halmashauri na kuyafanyia matumizi bila kupitia benki kwani ni kinyume na maelekezo ya serikali ya awamu ya tano.
Aidha, amewataka watumishi na madiwani wa halmashauri kuhakikisha wanashirikiana katika majukumu yao ya kila siku ili kutekeleza na kutimiza malengo ya halmashauri hiyo pamoja na maelekezo yote yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Simya alisema, ili kufikiwa malengo watumishi wa halmashauri kwa kushirikiana na madiwani wanapaswa kuwa wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato badala ya kubweteka kutokana na mafanikio waliyopata katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Juma Mnwele alisema, mwaka uliopita walikusanya bilioni 2.9 sawa na asilimia 94 na mwaka huu hadi kufikia mwezi Novemba tayari wamekusanya shilingi bilioni 1.6 sawa na asilimia 100 ambapo muelekeo wa makusanyo ya mapato ni mazuri na wana uhakika yatakuwa makubwa zaidi ya mwaka jana.
Alisema, watumishi wana hali kubwa ya kufanya kazi ikiwemo jukumu la kukusanya mapato ya ndani ambayo ndiyo uti wa mgongo wa halmashauri sambamba na kudhibiti matumizi ya fedha zinazokusanywa.
Mnwele alisema, kama mkurugenzi wa halmashauri ana matumaini makubwa na madiwani wapya, na amewakumbusha madiwani hao kuhakikisha wanazingatia viapo vyao vya maadili na kuepuka kutoa matamko ambayo yanaweza kuirudisha nyuma halmashauri yao.
Alisema, wao kama watendaji wa shughuli za kila siku watakuwa daraja zuri kati ya madiwani na wananchi na kuwaomba kuwapa ushirikiano mkubwa watumishi waliopo ili waweze kutimiza wajibu wao kwa maslahi ya halmashauri,wilaya,mkoa na taifa.
Kwa upande wake mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo Desdelius Haule alisema,kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha anashirikiana na madiwani wenzake kwa kila jambo ili kuharakisha maendeleo na uchumi wa Mbinga.
Alisema, madiwani wako tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa watumishi wa halmashauri hiyo ili kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu,wajibu wao na kuwahudumia wananchi ambao wana hamu kubwa ya kupata maendeleo hasa kufuatia serikali kuhamishia makao makuu ya halmashauri eneo la Kihamili kutoka Mbinga mjini.
Alisema, suala la ushirikiano kati ya madiwani,watumishi na wadau wengine ni jambo la maana kubwa kwani bila ya ushirikiano hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika katika suala zima la kuleta maendeleo.