Mnec Salim Abri akimpongeza Meya Ibrahim Ngwada
Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada akizungumza Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Manispaa Iringa.
*****************************************
NA DENIS MLOWE,IRINGA
MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa Iringa wamemwomba radhi mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (Mnec) Salim Abri kutokana na maneno mbalimbali aliyokuwa akitupiwa na baadhi ya wanachama na madiwani wa manispaa.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wote wakati wakufunga mafunzo kwa madiwani wa manispaa ya Iringa, Meya wa manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alisema kuwa kitendo cha kuomba radhi kinatokana na maneno mbalimbali ambayo amekuwa akitupiwa Mnec Salim Abri yaliyosababishwa na madiwani wenyewe katika kipindi cha mchakato wa kumtafuta Meya na Naibu meya wa Iringa.
Ngwada alisema kuwa kama kutupiwa matusi na maneno machafu yamesababishwa na madiwani wenyewe kwenye jimbo la Iringa mjini kutokana na homa ya uchaguzi wa nafasi hizo za umeya na unaibu meya hali ambayo imewalazimu kumwomba radhi mnec.
“ Tunaomba tuchukue nafasi hii kukuomba sana radhi kwani sisi kama madiwani wenzangu wamenituma nisimame mbele yao na mbele ya viongozi wa chama kukuomba sana radhi na kama umetukanwa sana kwenye jimbo letu, umedhalilishwa kwa namna yoyote na kama umeumia na familia yako imeumia katika kipindi hichi cha uchaguzi ni sisi madiwani” alisema na kuongeza kuwa
“ tumekutukana sisi wenyewe madiwani, tumewatuma watu wakutukane na kukukashfu na hivyo hatuna sababu zilizopelekea kufanya vile lakini tunasema tusamehe sisi”
Aliongeza kuwa wameomba radhi kwa kuwa wamemjeruhi yeye kama yeye na familia yake, biashara anazofanya hivyo kutokana na kitendo hicho madiwani wote wameomba radhi na kilichobaki ni kuungana na kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wanamanispaa ya Iringa.
Aidha walimwomba Mnec Salim kuwaombea radhi kwa viongozi wa CCM wilaya na Mkoa kwa kuhusisha maneno machafu kwenye mchakato wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya kitu ambacho hawakustahili kuhusishwa.
Ngwada aliongeza kuwa pamoja na mambo mbalimbali yaliyojitokeza kwa kiwango kikubwa kipindi cha mchakato wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wametambua makosa , wamejutia makosa na kwa pamoja wameamua kushikamana na kuondoa tofauti zote zilizojitokeza.
Alisema kuwa wameamua kuwa wamoja katika kusaidiana kuleta maendeleo ya kata zote na endapo diwani yoyote ataleta mtengano na maneno ya kuwavuruga na kugawa kwa pamoja vilevile watamgeukia na kuwa kinyume na yeye na kuanzia sasa zitasikika pilikapilika za maendeleo.
Aidha Meya Ngwada alitumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza mnec Salim Abri kwa kuwa na moyo wa kujitolea katika kusaidia na kufanikisha ushindi wa kishindo wa CCM Nyanda za Juu Kusini kutoka na majukumu aliyopewa kipindi cha uchaguzi na chama.
Kwa upande wake Mnec Salim Abri alipokea radhi hiyo kwa mikono miwili na kuwataka madiwani kuijenga Manispaa na Kuwaletea Wananchi Maendeleo waliyokuwa wakisubiri kwa kipindi kirefu.
Alisema kuwa wakati anakuja kufunga mafunzo hayo alikuwa anawaza vya kuzungumza kuhusu madiwani lakini kutokana na maneno yaliyotolewa na madiwani wote ya kuomba radhi hakika kwa mwanasiasa mkongwe hayo sio majeraha hivyo amesamehe kwa moyo mkunjufu.
Alisema kuwa kuna wakati zikipita wiki moja au mbili hajatupiwa maneno huwa anapata wasiwasi au amepoa lakini akianza kusemwa tu hapo mambo yanakuwa barabara kabisa kwani kwenye siasa ukiwa husemwi wala kuzungumzwa lazima hujitafakari kwani kuna kusemwa kwa ubaya au uzuri.
“Kuna msemo mmoja ulikuwa unatembea sana kwenye mitandao ya kijamii kama wewe ni kiongozi na unataka kila mtu akupende acha siasa kauze ice cream hivyo mimi siwezi kuacha siasa nikauze yoghurt wakati nimechagua siasa.” Alisema
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza madiwani wote waliochagulia na kuwahakikishia kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kuwapa misaada mbalimbali katika kata zao kwa kila mmoja pale ambapo watahitaji.
Aidha alisema kuwa changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa madawati, madarasa atahakikisha wanayamaliza kwani imekuwa kila mwaka yanajitokeza hali ambayo inemuumiza sana akili hivyo kwa kuwa manispaa iko chini ya CCM watahakikisha wanamaliza changamoto hiyo.