Medard Geho (aliyesimama) akitoa elimu kuhusu uthamini wa mashine na mitambo kwa watalaam wa uthamini katika Mafunzo ya siku moja yaliyotolewa Jijini Dar es Salaam ili kuwajengea uwezo.
Washiriki wa Mafunzo maalum ya uthamini wa mitambo na mashine wakifuatilia kwa makini mada kuhusu upekee wa uthamini wa mitambo na mashine, mada iliyotolewa na Dkt. Medard Geho (hayupo kwenye picha) Jijini Dar es Salaam.
Sultan Mndeme, mthamini aliyesajiliwa na mshiriki wa Mafunzo ya uthamini wa mitambo na mashine akichangia mada katika Mafunzo ya siku moja yaliyotolewa kwa wathamini Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo.
****************************************
Na: Eliafile Solla
Katika ukuaji wa uchumi wa nchi ya Tanzania, uthamini una nafasi maalum kama ilivyo kwenye nchi zote zilizoendelea. Kauli hii imetolewa Jijini Dar es Salaam na Dkt. Medard Lucas Geho kutoka White Knights Investiment Analysts Co. Ltd, alipokuwa akitoa elimu kwa wathamini kuhusu uthamini wa mitambo na mashine kwenye mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo watalaam hao. Dkt. Geho alisema, Tanzania inavyoingia kwenye uchumi wa viwanda, ni lazima uthamini ufanyike kwa kufuata uhalisia na misingi ya taaluma ya uthamini ili kusaidia usimamizi mzuri wa mitambo na mashine kwenye viwanda, uzalishaji mzuri wa malighafi na pia kusaidia viwanda kuongezeka.
Mafunzo haya ya uthamini wa mitambo na mashine yameratibiwa na Bodi ya Usajili wa Wathamini kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam wa uthamini ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuelekea uchumi wa viwanda. Pia Mafunzo haya yameendeshwa kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa bodi ya usajili wa wathamini ambapo tangia bodi hii ilivyoanzishwa, haya ndiyo mafuzo yake ya kwanza ya kuwajengea uwezo wataalam wa uthamini.
‘‘Hata katika nchi za Marekani na Ulaya, kuna wakati uchumi wao huwa unaporomoka kutokana na suala zima la uthamini na hasa wakati wa kutoa mikopo kwa kuweka rehani ya mali. Changamoto kama hizi zinatokea pale uthamini unapofanyika na thamani kuonekana iko juu kisha baada ya kuchukua mkopo mali iliyowekwa rehani inakuwa haiuziki na hivyo kusababisha hasara kwa Taasisi ama Shirika lililotoa mkopo. Ni muhimu mara zote kuhakikisha uthamini uko sahihi na hii ndiyo sababu tunatoa mafunzo ili kuwajengea uwezo wataalam wa uthamini hasa katika kipindi ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda; alisema Dkt. Geho’’
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Wathamini Bibi Edith Ushiwa amesema, mafuzo haya yametolewa kwa wataalam wa uthamini kama hatua ya awali ya kuwaandaa wakati Tanzania ikielekea katika uchumi wa viwanda. Hii ni kutokana na uhalisia kwamba, viwanda na mitambo ni vya gharama na hivyo ni lazima uthamini wake uwe makini na ufuate misingi ya taaluma ya uthamini. Katika uanzishwaji wa viwanda na ununuzi wa mitambo, wathamini watahusika kwa asilimia kubwa kwenye kufanya uthamini wa gharama za uwekezaji na mitambo itakayotumika kuendesha viwanda hivyo. Ushiwa aliongeza kwamba, uthamini ni dhana pana sana na hivyo wameamua kutoa mafuzo kwenye kipengele cha uthamini wa mitambo na mashine kwani kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuwa na uchumi wa viwanda.
Mafunzo ya uthamini wa mitambo na mashine yaliyotolewa kwa watalaam wa uthamini, yatawasaidia kuboresha kazi zao za uthamini na kugundua vipengele muhimu vya kuangalia wakati wa kufanya uthamini katika mitambo na mashine na hasa kusimamia miongozo ya taaluma zao kwa mujibu wa sheria ya uthamini.