******************************************
Na Immaculate Makilika-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka mawaziri kutoogopa kufanya maamuzi kwa kuogopa kufanya uamuzi mabaya.
Akizungumza leo, Ikulu Chamwino Dodoma mara baada ya kuwaapisha mawaziri 21 na manaibu waziri 22, Rais Magufuli alisema sasa mawaziri wanatakiwa kufanya maamuzi bila kuogopa kukosea. “Ni vizuri ukafanye uamuzi mbaya kuliko kutokufanya uamuzi, unashindwa kutoa uamuzi kwasababu hutaki uonekane mbaya, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita miradi ya maji zaidi ya 1,400 imekamilika, kwa hiyo mkafanye kazi, kafanyeni uamuzi hasa unaohusu maslahi ya taifa”, alisema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli amewataka mawaziri na viongozi wa Serikali kuzingatia uadilifu na kuhakikisha kuwa maagizo na maelekezo ya Serikali yanafuata utaratibu. “Ndani ya Serikali sasa hivi kuna ugonjwa mmoja wa ajabu, kwamba hata mawasiliano yanatumwa kwenye ‘group za WhatsApp, barua nyingine ni za siri na zinaishia kuvuja. Tuzingatie maadili ya viapo vyetu na tufanye kazi zetu kwa uadilifu mkubwa, Serikali hufanya kazi kwa maandishi”, alisisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu somo la historia, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa somo hilo linakuwa somo la lazima kufundishwa mashuleni ili wanafunzi waweze kujua historia ya nchi yao.
“Nataka wanafunzi wetu wafundishwe historia ya Tanzania na hii itasaidia kujenga uzalendo, vijana hawajui historia ya nchi yetu, inawezekana masomo haya yatasaidia kujua jinsi wageni walivyokuja wakadanganya wazee wetu”, alisisitiza Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizungumzia changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo matumizi mabya ya fedha za umma ambapo alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha yaliyofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kununua gari la gharama ya zaidi ya shilingi milioni 400.
Halikadhalika, Rais Magufuli alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita vijiji 9,880 vilipata umeme na katika kipindi cha miaka mitano ijayo vijiji 2,338, vilivyobaki pia vipate umeme, sambamba na kuanza mradi wa uzalishaji megawati 350 za umeme wa maji mkoani Njombe zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Vilevile, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa kuhakikisha kero za wasanii na wanamichezo zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kusaidia wasanii kupata haki zao.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwataka mawaziri kafanya kazi kwa bidii, ili kutimiza matumaini ya wananchi katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Naye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa mawaziri, wameapa kumsaidia mhe. Rais kazi na jukumu kubwa ni kufanya kazi kwa kuwatumikia watanzania. “Tunahitaji kuona matokeo ya kazi maana miongozo tayari tunayo. Twende tukachape kazi”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.