Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James akizungumza wakati wa hafla ya kusaini kwa mkataba baina ya Tanzania na Korea utakaoiwezesha serikali kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi wa Korea.
Balozi wa Korea nchini, Cho Tae-Ick akizungumza baada ya kusaini mkataba huo baina ya nchi yake na Serikali ya Tanzania leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James (katikati) na Balozi wa Korea Nchini Cho Tae-Ick (kulia) wakisaini mkataba utakaoiwezesha Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu.
……………………………………
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea zimetiliana saini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu kutoka mfuko wa ushirikiano wa kiuchumi (EDCF) yenye thamani ya shilingi bilioni 684.6 kwa ajili ya kugharamia miradi ya Nishati, Maji, bajeti ya Seriakali na Ujenzi.
Akizungumza mara baada ya kutiliana saini mkataba huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango bwana Dotto James amesema mkopo huo wa dola za kimarekani milioni 300 ambazo ni sawa na Bilioni 684. 6 ni wa masharti nafuu utakao kwenda kusaidia katika miradi ya maendeleo na bajeti kuu ya Serikali.
Ametaja baadhi ya miradi ya maendeleo itakayowezeshwa na fedha hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya kupozea umeme katika njia ya kusafirisha umeme ya Kigoma, Nyakanazi.
“Mkopo huu utakwenda kusaidia ujenzi wa vituo viwili vya kupozea umeme katika njia ya kusafirisha umeme ya Kigoma- Nyakanazi (Grid ya taifa ya kaskazini Magharibi) utakaogharimu dola za Marekani milioni 45, sawa na shilingi bilioni 102.9” amesema James.
Amesema pia fedha hizo zitakwenda kusaidia bajeti kuu ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 91.4 ili kuziba pengo la kibajeti lililotokana na madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID 19) lengo ni kuboresha mfumo wa Afya hapa nchini kwa kuongeza uwezo wa bajeti ya Serikali.
Pia amesema katika ya fedha hizo zitakwenda kuboresha huduma ya mfumo wa maji taka katika jiji la Dodoma kwa kujenga mtambo wa kutibu maji taka na kupanua wigo wa mabomba ya maji taka na kuongeza idadi ya watu wanaoweza kupata huduma hiyo.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa mtambo wa kutibu maji taka wenye uwezo wa mita za ujazo elfu 20 kwa siku, ujenzi wa mfumo wa maji taka kuunganisha mabomba ya mfumo wa maji taka na majengo ya ofisi” amesema.
Mradi mwingine ni kuimarisha miondombinu ya upimaji na ramani ambapo shilingi bilioni 148.6 zitatumika mradi huo unalenga kuimarisha na kuboresha miondombinu ya upimaji wa ardhi na ramani kusaidia kujenga uwezo endelevu wa Serikali wa kuandaa ramani za msingi.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa vituo 30 vya upimaji ardhi vya kielektroniki katika miji mikuu ya Mikoa na kuongeza alama 357 za upimaji ardhi nchini na kuongeza vituo kufikia 33 na alama 985, kupatikana kwa vifaa vya kuandaa ramani, kujenga kanzi data za taarifa za kijiografia” amesema.
Mradi mwingine ni ujenzi wa daraja jipya la Selander ambapo shilingi bilioni 74.5 zitatumika kuendeleza ujenzi wa daraja hilo ambapo awali dola za kimarekani milioni 91.032 hazikutosha kukamilisha mradi huo kutokana na gharama kuongezeka lengo ni kupunguza foleni katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi Dar es saalam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa serikali ya Tanzania hasa katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ambapo jumla ya bilingi bilioni 589.86 zimetumika katika miradi mbalimbali.
Kwa upande wake balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchi Mheshimiwa Cho Tae-Ick amesema ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni wa mda mrefu na wataendelea kushirikiana katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo katika jitihada ya kuinua uchumi wa hapa nchini.
Amesema Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na kusema ni jukumu la Tanzania kutaja maeneo yanayohitaji uwekezaji ili washirikiane kuongeza nguvu katika sekta ya uwekezaji hapa nchini.