**********************************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta amewataka mafundi simu mkoani hapa kuhakikisha wanashiriki mafunzo mahiri ya simu yatakayowajengea uwezo ili kuepuka vitendo vya uhalifu wa kutumia simu kama takwa la kisheria linavyoelekeza.
Aidha Kimanta ameonya kwa yeyote atakayepatikana akifanyakazi ya kutengeneza simu bila kupitia mafunzo hataruhusiwa kufanyakazi hiyo na atachukuliwa hatua za sheria .
Akiongea wakati akifungua mafunzo maalumu kwa mafundi simu katika mikoa ya kanda ya kaskazini, yaliandaliwa na TCRA na Veta, na kufanyika jijini Arusha
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa mafunzo hayo sio ya hiyari bali ni lazima kwa Kuwa yanalenga kuwajengea uwezo, weledi na ufanisi kwa mustakabali wa usalama wa Taifa.
Aidha Kimanta ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha inasimamia sekta ya mawasiliano kikamilifu ili mafundi wote wapitie mafunzo hayo sanjari na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuondoa vishoka .
“Nitoe wito kwa mafundi simu mjue kwamba kazi ya kutengeneza simu ni ajira ya kujipatia kipato ,lakini maagizo ya serikali ni kuwapatia mafunzo nchi nzima, ninachotaka kwenu kuweni waaminifu wakati wa Kutekeleza wajibu wenu”alisema Kimanta
Awali mkurugenzi mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bukulu alisema kuwa mafunzo haya yanalenga kuboresha matengenezo ya simu za mkononi usalama wa simu za mkononi na usalama wa data zinazotunzwa kwenye simu hizo usalama wa mtumiaji wa simu za mikononi
Alisema kuwa kwa ujumla matumizi sahihi ya simu za mkononi yakiongezeka yanaongeza tija katika ujenzi wa uchumi na kuleta maendeleo chanya kwa taifa hivyo mafunzo hayo ni muhimu sana kwani ongezeko la simu zaidi ya milioni 45 zinatumika maeneo mbalimbali zimeenea kwa asilimia 65 nchini.
Alibainisha kwamba mafunzo hayo yanaonyesha umuhimu mkubwa wa mafundi hao kwani inaonyesha jinsi ujuzi wao unavyohitajika kwenye jamii.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini TCRA Mhandisi James Kilaba alisema kuwa lengo la mafunzo hayo yanayotolewa na veta kwa mafundi simu ni kutekeleza malengo mkakati wa udhibiti wa TCRA.
Alisema kuwa watumiaji wa simu za mkononi kwa nchi yetu ni zaidi ya milioni 45 hivyo mafundi simu ,wenye weledi na ujuzi wanahitajika kufanya matengenezo pindi zinapoharibika, ndio maana TCRA imeamua kushughulikia jambo hilo baada ya kubaini mafundi wengi hawana ujuzi unaoendana na teknolojia ya habari na mawasiliano.