***************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Des 3
MKUU wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi Shule ya Msingi Chatembo iliyopo kata ya Mwandege ,Wilayani Mkuranga,inayojengwa kwa gharama ya Sh.Milion 400, Fedha kutoka Serikalini.
Kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia watoto wa maeneo jirani kupata elimu karibu pasipo kuifuata mbali na kujiinua kitaaluma.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Ndikilo pia aliwataka Wakuu wa Wilaya Mkoani hapo kuhakikisha wanafunzi 30,197 waliofaulu Darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuwa wanaripoti shuleni shule zitakapo funguliwa Januari 11,2021.
Amesitisha likizo za wakuu wa Wilaya wote, wakurugenzi nakuitaka Sekretariet ya Mkoa kutembelea Halmashauri zote na kukagua ujenzi Miundombinu, ili kuhakikisha Miundombinu yote inapatikana na wanafunzi wote hawa wawe madarasani ifikapo January 11,2021.
Ndikilo aliishukuru serikali kwa kuupatia ,Mkoa huo takribani Shilingi Bilioni 16.5 kwa ajili ya uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu na Ukarabati wa Shule Kongwe.
Aliwataka Meneja wa Shirika la Umeme na Maji Wakala wa Barabara TARURA Wilayani Mkuranga kufikisha umeme kwenye shule hiyo Mpya ya Chatembo.