Naibu Mkurugenzi Mkuu wa wa TanTrade Bi.Latifa Khamis akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam juu ya Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania ambayo yanatarajiwa kuanza Desemba 3 hadi 9,2020.
******************************************
NA MWANDISHI WETU
Wafanyabiashara na wenye viwanda wametakiwa kujitokeza katika Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yatakayoanza tarehe 3 hadi 9 Desemba, 2020 katika Viwanja vya Maonesho Sabasaba, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda unakuwa na matokeo chanya katika uchumi na yanayoonekana.
Akizungumza hivi karibuni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi.Latifa Khamis amesema Maonesho hayo yanalenga kujenga jukwaa kwa Wadau wa Sekta ya Viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo katika Sekta hiyo.
“Maonesho haya yanahamasisha Watanzania kutumia bidhaa zao kama kauli mbiu inavyosema“Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania” na hii kauli mbiu tumeiweka mahususi tunataka nao Watanzania wawe wazalendo”.Amesema Bi.Latifa.
Aidha Bi.Latifa amesema bidhaa nyingi za Watanzania zimeboreshwa na zinaweza kushindana na bidhaa nyingine hivyo watanzania wanatakiwa kuendelea kupenda bidhaa zao.
Hata hivyo amesema mbali na maonesho pia kutakuwa na mikutano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na wamiliki wa Viwanda ambao utasimamiwa na Wizara hiyo pia kutakuwa na taasisi ambazo zinasimamia mnyororo mzima wa biashara na udhibiti wa masuala mbalimbali ya biashara na viwanda.
Hivyo basi Bi.Latifa ametoa wito kwa wenye viwanda na wafanyabiashara kwa ujumla kushiriki katika mkutano huo ambao utafanyika Desemba 5, 2020 kwani kupitia mkutano huo wataweza kukutana na wakuu wa taasisi mbalimbali na watapata fursa ya kuongea na kusema changamoto zao na kutatuliwa.