………………………………………………………………………………..
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Kuelekea katika siku ya walemavu duniani ambayo huadhimishwa Disemba 3, kila mwaka jamii imetakiwa kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu bali ione watu wenye ulemavu nao ni miongoni mwa jamii inayotakiwa kupata fulsa sawa na watu wengine.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na mwenyekiti wa shirika la Foundation for disabilities hope Bw.Michael Silari wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea siku hiyo ambayo kitaifa itafanyika Dodoma amesema bado kundi la watu wenye ulemavu linaachwa nyuma na jamii na kuona kama sio miongoni mwa jamii.
“Tunatoa wito kwa jamii kuona kundi hili nalo ni miongoni mwa jamii na ndio maana hata haya maadhimisho huwa tunapeleka katika mikoa mbalimbali ili kupanua uelewa wa jamii juu ya watu wen ye ulemavu” amesema Silari.
Amesema siku hiyo iliwekwa kwa lengo la kuwaunganisha watu wenye ulemavu na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu na kujadili kwa pamoja mambo hayo ili kujenga umoja miongoni mwao.
Amebainisha kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazolikabili kundi hilo kwani jamii huliona kundi hilo kuwa haliwezi jambo lolote bali walemavu ni kama watu wengine na wanatakiwa kushirikishwa katika mambo mbalimbali yanayoizunguka jamii.
Amesema changamoto nyingine ni watu wenye ulemavu wenyewe kujinyanyapaa na kuona hawawezi kitu chochote amewataka kubadilika kwani nao ni miongoni mwa watu katika jamii wanaotakiwa kuleta maendeleo kama watu wengine.
“Watu wenye ulemavu wenyewe wamekuwa wakijinyanyapaa na kuona kama sio miongoni mwa jamii nataka wajiamini kwani nao ni miongoni mwa jamii inayotegemewa kuleta maendeleo katika jamii” amesema.
Ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaanini watu wenye ulemavu na kuwateua katika nyanja mbalimbali za uongozi sambamba na kutenga asilimia 2 za makusanyo ya halmashauri kwa ajili kuwawezesha watu wenye ulemavu kuwainua kiuchumi.
“Tuishukuru serikali kwa kuendelea kutuamini imeteua watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali na tunaona watu wenye ulemavu wamefanya vizuri katika kazi hizo na sisi kama shirika tutaendelea kushirikiana na serikali katika kuhimiza watu wenye ulemavu kujitokeza kwenye mikopo hiyo” amesema.