*******************************
NA EMMANUEL MBATILO
Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za binadamu ya mwaka 2019 iliyotolewa na kituo cha Sheria na Haki za binadamu zaidi ya Matukio 42,824 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa Polisi kwa mwaka 2016 hadi 2019.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam katika hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kikazi baina ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na Taasisi ya Jamii Forums ili kukuza uelewa wa hali na ustawi wa mtoto wa Kitanzania katika harakati za kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.
Akizungumza baada ya kuingia makubaliano Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti amesema wameamua kushirikiana na Jamii Forums kwa lengo la kuhakikisha wanapaza sauti kwa jamii ili kukomesha vitendo vya kikatili kwa watoto hasa wa kike ikiwemo mimba za utotoni,ukeketaji,ndoa za utotoni,ulawiti pamoja na ubakaji
Aidha amesema Utafiti wa Demographia na Afya (TDHS) wa mwaka 2015/2016 unaonyesha asilimia 27 ya wasichana kati ya miaka 15 hadi 19 walipata ujauzito. Kwa mwaka 2003 hadi 2011, wanafunzi 55 elfu waliacha shule kwa sababu ya mimba za utotoni, wengi wakiwa kati ya umri wa miaka 13 hadi 18.
“Kwa kipindi cha Januari 2018 hadi Desemba 2019, LHRC ilikusanya matukio zaidi ya 2543 ya mimba za utotoni. Lakini tunaamini matukio mengi zaidi hayajaripotiwa”Alisema Mtngeti.
Hata hivyo amedai Nchini Tanzania, ukeketaji ni kosa la jinai katika sheria ya kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 (kifungu 169A), lakini bado baadhi ya jamii zimekuwa zikifanya ukeketaji wa watoto wa kike huku Ukeketaji ukipungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi asilimia 10 kwa mwaka 2016 kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali, asasi za kiraia na wadau wengine wanaopinga ukeketaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Jamii Forums Maxence Melo amesema kupitia mtandao wao watahakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga jamii yenye uelewa wa mambo anuai.
Hata hivyo ikiwa bado ni muendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo huanza rasmi Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka Taasisi ya CDF na Jamii Forum zitashirikiana katika kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia hasa ukatili wa kingono.