Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Uvuvi wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala ya kipaumbele ya Mpango Kabambe unaofanyika Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.
Sehemu ya Wadau wa Sekta ya Uvuvi wakiwa makini kufuatilia matukio katika Mkutano wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala ya kipaumbele ya Mpango Kabambe unaofanyika Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.
…………………………………………………………………………….
Na Mbaraka Kambona, Singida.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mchakato wa kukamilisha Mpango kabambe wa miaka 15 ijayo kuanzia 2021 utakaosimamia sekta ya Uvuvi na kutoa dira ya kulinda rasilimali za uvuvi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa na endelevu katika pato la taifa.
Hilo limefahamika wakati Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Uvuvi wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala ya kipaumbele yanayopaswa kuingizwa katika Mpango huo Kabambe unaofanyika Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa lengo la Serikali ni kuona sekta ya Uvuvi inaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa zaidi ya ilivyosasa na ndio maana inaanda Mpango huo ili usimamizi wa rasilimali za uvuvi uwe imara.
“Ni mategemeo yetu kuwa mpango huu utatoa hamasa kwa sekta ya uvuvi katika kulinda usalama wa chakula kuanzia ngazi ya kaya na taifa, vilevile tunatarajia utuingize katika uchumi wa viwanda na uchumi wa bluu,” alisema Dkt.Tamatamah
Alisema kuwa pamoja na juhudu za Wizara za kusimamia maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini, Sekta hiyo imeendele kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa ujumla zimekuwa zikiathiri ukuaji na uendelevu wa sekta hiyo.
Aliendelea kueleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imekuwa ikitekeleza mipango, mikakati na programu mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya uvuvi nchini, miongoni mwa mipango hiyo ni Mpango huo Kabambe wa Uvuvi unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka 2021.
Mratibu wa Masuala ya Uvuvi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ambao wanafadhili maandalizi ya mpango huo, Dkt. Oliver Mkumbo alisema shirika hilo limeamua kufadhili mpango huo ikiwa ni sehemu ya malengo yao ya kuhakikisha dunia inaondokana na njaa, umasikini na kuimarisha usalama wa chakula ili ifikapo mwaka 2030 pasiwepo na mtu atakayekuwa na njaa.
Aidha, wadau wa Sekta ya Uvuvi hawakusita kuonesha matumaini yao na mpango huo huku wakisema kuwa ukikamilika utajibu changamoto nyingi ambazo zimeendelea kukabili sekta hiyo.
Kiongozi wa Wavuvi Mkoani Kigoma, Francis John alisema kuwa mpango huo ambao utasimamia rasilimali za uvuvi utawasaidia kuimarisha biashara yao ya dagaa kutoka ziwa Tanganyika kwani mpango huo utawahakikishia uwepo wa dagaa wengi ambapo wataweza kuwa na mzigo wa uhakika wa kusafirisha kwenda kuuza dagaa wao katika nchi za Marekani, Astralia, Kanada, Uingereza na Denmark.
Naye, Raphael John, mdau wa sekta hiyo ya Uvuvi alisema kuwa moja ya mambo yatayokwenda kuimarishwa kupitia mpango huo ni ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji jambo ambalo anasema litasaidia kupunguza utegemezi wa kupata mazao ya uvuvi kutoka maji ya asili pekee.
“Katika nchi nyingi zilizoendelea, ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji umepewa kipaumbele sana, ni muhimu kuimarisha eneo hilo ili tusitegemee tu uvuvi wa mazao ya samaki katika maji ya asili, ni lazima tuanze sasa kabla rasilimali za asili katika bahari, mito na maziwa hazijaisha,” alisema John
Mpaka sasa sekta ya uvuvi inachangia asilimia 1.7 katika pato la Taifa huku ikielezwa kuwa sekta hiyo inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wananchi takriban 202,000 na wananchi wengine wasiopungua Milioni 4.5 wamaendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia sekta hiyo.
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetoa Dola za Kimarekani 195,000 kwa ajili ya kufanya mapitio na kuandaa Mpango huo Kabambe wa sekta ya uvuvi ili sekta hiyo iweze kusimamiwa vizuri na kuendelea kuleta maendeleo yenye tija nchini.
Uandaaji wa mpango huo ni sehemu ya mipango mingi ambayo serikali imekusudia kuitekeleza, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 13, 2020 jijini Dodoma, Mhe. Rais, Dkt. John Joseph Magufuli alieleza mipango kadhaa ya kuboresha sekta ya uvuvi ikiwemo ununuzi wa meli nane (8), ujenzi wa Bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira elfu thelathini (30,000).