Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akikaribishwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, kuzungumza na Wananchi wa Munzeze alipotembelea Kata ya hiyo iliyopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Mkazi wa Kijiji cha Munzeze, wilayani Buhigwe, Kigoma, Bw. Maxmilian Joseph, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata ya Munzeze, mkoani humo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Wananchi wa Kata ya Munzeze, ambapo ameahidi kutafuta namna bora ya kuhakikisha zao la Tangawizi linaongezewa thamani na kutafutiwa soko la uhakika ili kuinua uchumi wa wananchi wa Kata hiyo, mkoani Kigoma.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Munzeze, wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, (hayupo pichani), ambaye amewaahidi kutatua kero ya soko la Tangawizi pamoja na ujenzi wa shule ya Sekondari katika kata hiyo. Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akicheza ngoma na vikundi vya Upendo na Mkombozi, alipotembelea Wilaya ya Buhigwe, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kishindo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na yeye binafsi wakati wa uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani) njia ya kuwasaidia wananchi wa Kata ya Muzeze, Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, kuondokana na umasikini kwa kuongeza thamani ya zao la Tangawizi linalolimwa kwa wingi na wananchi hao.
Mkazi wa Kata ya Munzese Bw. Yohane Petter, akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani) kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifungashio vya kisasa vya zao la Tangawizi ili zisiharibike haraka.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Madiwani wa Jimbo la Buhigwe baada ya kuhutubia wananchi wa katika Ofisi za CCM Wilaya ya Buhigwe, tarafa ya Manyovu, mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiteta jambo na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Munzeze Bw. Msaki Emmanuel alipotembelea kituo hicho kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.
Diwani wa Kata ya Munzeze Mhe. Wilson Vyabhoze, akimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye ni Mbunge wa Buhigwe, kwa kuchaguliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa mara nyingine na kuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake kwenye Kata hiyo iliyopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.
(Picha na Josephine Majura – Wizara ya Fedha na Mipango-KIGOMA)
**********************************
Na Josephine Majura, Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, ameahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la soko la zao la biashara la Tangawizi linalolimwa kwa wingi Kata ya Munzeze wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.
Dkt. Mpango ametoa ahadi hiyo katika Kata ya Munzeze mkoani Kigoma, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo ambapo amesema atatafuta masoko ndani na nje ya nchi ili wananchi wa mkoa wa Kigoma waweze kufaidika na kilimo cha zao hilo la biashara linalotegemewa na wananchi wengi kujipatia kipato.
“Nikiwa kwenye kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu nilishuhudia wafanyabiashara kutoka nchini Burundi wakinunua Tangawizi mbichi kwa bei ya chini na kuipelekea Tangawizi hiyo nchini mwao na kuichakata kisha kutuletea hapa nchini na kutuuzia kwa bei ya juu, hili halikubaliki, sisi tunatakiwa kuongeza thamani ya Tangawizi na kuiuza nchini mwao” alisema Dkt. Mpango
Sambamba na hilo Dkt. Mpango, aliwaahidi wananchi wa Kata ya Munzeze kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule ya Sekondari Kigogwe inayojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuboresha elimu katika Kata hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, alisema kuwa Wilaya yake inakabiliwa na lindi la umasikini kwa wananchi wake na kumwomba Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, Mhe. Dkt. Philip Mpango, kuwasaidia wananchi wa Wilaya hiyo kuondokana na hali hiyo kwa kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo zao la Tangawizi
Alieleza kuwa changamoto ya bei ya zao la Tangawizi inamsononesha kwani wananchi hususani wa Kata ya Muzeze ambao ni wakulima wazuri wa Tangawizi wanauza kilo moja ya zao hilo kwa kati ya shilingi 400 hadi shilingi 700, bei ambayo ni ndogo na haiwanufaishi wakulima.
“Nimeingia kwenye mitandao kutafuta mashine za kuongeza thamani ya zao la Tangawizi ambapo nimeona kuna mashine za kuosha Tangawizi, kuchambua, kuchakata na kufungasha zao hilo na zana hizi zikipatikana kwa wananchi wa Munzeze wataondokana na changamoto hiyo ya kuuza Tangawizi ghafi kwa bei ya hasara” Alisema Kanali Ngayalina
Naye Diwani wa Kata ya Munzeze Mhe. Wilson Vyabhoze, amemuomba Waziri wa Fedha na Mipango, kuona namna ya kuanzisha Taasisi ambazo zitakuwa zinauza mbegu za mazao mbalimbali likiwemo Tangawizi ili kuwarahisishia Wananchi upatikanaji wake kwa kuwa ardhi yao ina rutuba ya kutosha.
Mkazi wa Kata ya Munzeze Bw. Yohane Peter amemuomba Dkt. Mpango kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifungashio vya kisasa vya Tangawizi ili zisiharibike haraka.
Katika ziara hiyo Dkt. Mpango ametembelea Kata ya Janda, ambapo Wananchi wa eneo hilo waliomba atatue changamoto ya Zahanati na kuahidi kushughulikia kwa haraka jambo hilo.
Vile vile Waziri Mpango, alitembelea Kata ya Bukuba ambapo aliahidi kumalizia ujenzi wa Zahanati mbili ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi hadi hatua ya renta kwa ajili ya kuhudumia Kijiji cha Bukuba na Kijiji cha Kibuye mkoani Kigoma.
Aidha aliongeza kuwa Serikali itajenga maabara katika Shule ya Sekondari ya Bwafuu ili kuboresha mazingira ya shule hiyo ili kutoa Wanafunzi wenye uelewa wa nadharia na vitendo katika masomo ya sayansi.
Dkt. Mpango aliwasisitiza Wananchi wa Munzeze kuendelea kudumisha amani na usalama wa nchi kwa kuwa ndiyo kitu muhimu katika maendeleo yoyote yale kwa kuwa Mkoa huo upo mpakani na nchi jirani ya Burundi
“Amani ni kitu muhimu sana kwenye maisha yetu ya kila siku, bila amani biashara haziwezi kufanyika, bila amani Watoto hawataweza kwenda shule, bila amani shughuli za kimaendeleo hazitaweza kufanyika, ndugu zangu tuendelee kuidumisha amani yetu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu”. Alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi na kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la Buhigwe kwa kumchagua kwa kura za kishindo, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeye binafsi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.
Katika ziara hiyo amepanga kutembelea Kata nane kati ya ishirini zilizopo kwenye Jimbo lake la Buhigwe mkoani Kigoma, hadi sasa ameshatembelea Kata tano ikiwemo Munanila, Mwayaya, Munzeze, Janda na Bukuba.