Na John Walter, Manyara
Jumuiya ya wazazi kupitia chama cha mapinduzi (CCM) imeeleza kuwa imejipanga kuanzisha shule za sekondari ambazo zitalenga kuwasaidia watoto na kuongeza mapato katika jumuiya hiyo ili iweze kujiendesha vizuri.
Akizungumza na wajumbe wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Manyara Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Dkt. Edmud Mndolwa, alisema awali Jumuiya hiyo ilikuwa na shule lakini hazikuwa nzuri kutokana na muongozo kuwa mbaya.
“Tuna kila sababu ya shule zetu kufanya vizuri kinachotakiwa ni kuwa na adabu na kufuata miongozo iliyopo hakuna usimamizi wowote uliofanikiwa bila kuwepo na adabu” alisema Mndolwa.
Mndolwa alisema mtu ambaye hatakubaliana na miongozo ya uendeshaji shule hizo watamuondoa mapema na pia ikitokea mtu akagundulika ni mbadhirifu wa fedha atashughulikiwa.
Alisema kwa sasa kitega uchumi cha Jumuiya hiyo ni shule pamoja na ufugaji wa nyuki na watahakikisha wanakuwa na shule bora katika kanda nane ambapo watahakikisha wanafuta daraja la nne na kubaki na daraja la kwanza kwa asilimia 80 na daraja la pili asilimia 20.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Manyara Fratern Kwaison alisema kuwa kama Jumuiya hiyo inahitaji shule kuna haja ya kuanzisha kuanzia mwanzo na siyo kuchukua shule zile ambazo zilishaanzishwa baadaye zikachukuliwa na serikali.