……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli,amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itatenga fedha kidogokidogo kwa ajili ya kuziandaa timu za taifa katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Pia Rais Magufuli ameitakia ushindi timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika mchezo wa leo dhidi ya timu ya Tunisia Mchezo wa Kufuzu Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika mwakani 2021 nchini Cameroon pamoja na Bondia Hassan Mwakinyo katika pambano la kuwania ubingwa wa WBF dhidi ya Bondia Carlos Paz wa Argentina.
Kauli hiyo ameitoa leo bungeni Dodoma wakati akizundua Mkutano wa kwanza wa Bunge la 12 sambamba na kulihutubia Taifa.
“Nitumie fursa hii kuitakia kila la heri timu yetu ya taifa dhidi ya Tunisia na bondia wetu Hassan Mwakinyo katika pambano lake baadaye leo hivyo Watanzania tunakata ushindi, kushindwa shindwa ” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameeeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya Sanaa, Utamaduni pamoja na Michezo kwani zimezidi kuimarika kwa kasi pia ameahidi kuhuisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ili kuwasaidia wasanii kupata mafunzo ya sanaa pamoja na mikopo.
Aidha Dkt.Magufuli amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itaimarisha usimamizi wa Hakimiliki za wasanii ili wanufaike na kazi zao pamoja na kuchangia pato la taifa.