Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua Gwaride la Heshma lililoandaliwa na Vikosi vya Jeshi la Polisi nchini mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kwa ajili ya kuhutubia pamoja na kulifungua rasmi Bunge hilo la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama wakati Wimbo wa Taifa ulipokuwa ukipigwa mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kwa ajili ya kuhutubia pamoja na kulifungua rasmi Bunge hilo la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameongozana na Spika wa Bunge Job Ndugai wakati akiingia ndani ya Bunge jijini Dodoma kwa ajili ya kuhutubia pamoja na kulifungua rasmi Bunge hilo la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia pamoja na kulifungua rasmi Bunge hilo la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya kufungua Bunge la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma. Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete mara baada ya kufungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 13 Novemba, 2020. PICHA NA IKULU
…………………………………………………………………………………
Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kulihamisha suala la uwekezaji ikiwemo Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na kuhami Ofisi ya Rais ili aweze kupambana vizuri na wanaokwamisha wawekezaji.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jijini Dodoma wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la 12 Mkutano wa Kwanza kikao cha Nne wakati akilihutubia bunge.
Aidha Rais Magufuli amesisitiza kuwa mtu mwenye mtaji anayehitaji kuwekeza katika Tanzania apate vibali ndani ya siku 14 ili uwekezaji huo kusaidia taifa ili kuendelea kimaendeleo.
“Miaka mitano iliyopita tuliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha nchi yetu kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa kwa kifupi niseme utumbuaji unaendelea”, ameeleza Rais Magufuli
Rais Magufuli amesema kuwa atashirikiana na rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kulinda Amani, hawatokuwa na utani hata kidogo na mtu atakaye taka kuvuruga Amani na kuingilia uhuru wa Tanzania.
“Namuahidi Rais Mwinyi nitampa ushirikiano wa kutosha katika kukamilisha aliyoyaahidi ili kutimiza adhima ya watanzania walio tuamini”, amesisitiza Rais Magufuli.
Lakini pia Rais Magufuli ameeleza kuwa Sekta ya utalii imeajiri watu takribani milioni nne kwenye miaka mitano iliyopita , sekta hiyo ilikuwa ikitoa mchango mkubwa ambao ulikuwa unaridhisha ambapo idadi ya watalii waliotembelea nchini iliongezeka pamoja na mapato pia.
“Naipongeza hifadhi yetu ya taifa ya Serengeti kwa kuchaguliwa kuwa hifadhi bora barani afrika mwaka huu”, amepongeza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa miaka mitano ya ya uongozi wake wa awamu ya pili watanunua meli nane za uvuvi ambapo meli nne zitakuwa Zanzibar nan ne Tanzania Bara ambapo zitafanya kazi kwenye bahari kuu.
Pia Rais Magufuli ameongeza kuwa serikali yake imepanga kupunguza foleni barabarani , itapanua viwanja vya ndege 11, kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme , itafikisha umeme kwenye vijiji vyote vilivyobaki, na upande wa afya itahakikisha watanzania wote wanakuwa na bima ya afya na kuongeza hospitali.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema kuwa Katika miaka mitano ijayo amepanga kuimarisha usafiri wa reli ya kati na TAZARA, kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Daer es salaam , Morogoro, hadi Dodoma.