Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akitoa hotuba ya ufunguzi mbele ya Makatibu Wasaidizi wa TSC (hawapo pichani) kutoka Wilaya mbalimbali za Tanzania Bara wakati wa Kikao cha Kazi cha Makatibu Wasaidizi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Moses Chitama akitoa maneno ya utangulizi kwa Makatibu Wasaidizi TSC (hawapo pichani) wakati wa Kikao Kazi cha Makatibu Wasaidizi wa TSC kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma.

Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya mbalimbali za Tanzania Bara wakiwa katika Kikao cha Kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma

Mweyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Willy Komba (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Makatibu Wasaidizi wakati wa kikao cha kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma. Wengine (waliokaa) ni Wakurugenzi kutoka TSC Makao Makuu.

………………………………………..

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba amewataka watumishi wa Tume hiyo kufanya kazi kwa bidii na weledi mzuri ili kuwezesha walimu kupatiwa huduma kwa wakati.

Prof. Komba wito huo ameutoa katika kikao kazi kilichowahusisha Makatibu Wasaidizi kutoka Wilaya zote za Tanzania bara kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Chuo cha Mipando jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha amesema kuwa wapo baadhi ya watumishi wa Tume ambao wamekuwa ni kikwazo katika ustawi wa walimu huku akisisitiza kuwa Tume ilianzishwa kwa lengo la kumsaidia mwalimu ili aweze kuwa na ustwawi mzuri katika utumishi wake.

Ameweka bayana kuwa kumekuwa na vitendo mbalimbali vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma kwa baadhi ya watendaji wa TSC huku akisisitiza kuwa katika kipindi cha uongozi wake hatomvumilia mtumishi yeyote asiyetaka kufanya kazi kwa mujibu wa Taratibu.

“Wapo baadhi yenu ambao tumepata taarifa zao na tumeanza kuwachukulia hatua kutokana na kutozingatia maadili ya kazi. Unakuta Katibu Msaidizi anaomba rushwa kwa mwalimu mwenye mashauri ya nidhamu ili hata kama ana hatia wasimpe adhabu”, ameeleza prof. Komba.

Ameongeza kuwa hata katika mchakato wa kuwapandisha madaraja walimu wapo baadhi ya watumishi wanaojihusisha na rushwa kwa lengo la kutoa upendeleo kitu ambacho sio kwamba tu ni kinyume na sheria lakini kinadhalilisha Utumishi wa Umma.

Katika kushughulikia mashauri ya nidhamu, prof. Komba amesema kuwa kwa kipindi ambacho amekaa Tume kama mwenyekiti amebaini kuwa zipo changamoto kwa Makatibu Wasaidizi na Kamati za Wilaya katika kuendesha  mashauri ya nidhamu kwa walimu.

“Nimeona rufaa zinakatwa na walimu kupinga maamuzi yanayofanywa na Kamati za Wilaya. Rufaa nyingi zinakubaliwa na uamuzi wa kamati za wilaya unatenguliwa lakini ukiangalia sababu kubwa za rufaa kukubaliwa ni kutozingatiwa kwa Kanuni na Taratibu wakati wa kuendesha mashauri”. Ameongezea Mwnyekiti huyo.

Alisema Tume imeamua kuendelea kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi katika kufahamu Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na Kanuni zake ili kuongeza weledi katika uendeshaji wa mashauri ya nidhamu wilayani.

Katika Mkutano huo mada mbalimbali zilitolewa zikilenga kuwajengea uwezo Makatibu hao katika masuala ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu, Maadili na Miiko ya Utumishi wa Walimu, Uwekaji Malengo ya Utendaji wa Kazi pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Walimu nchini.