**************************************
– Hakukubali kushindwa, wala kuinua simu kumpigia mshindi
Ni utamaduni wa Wamarekani wa miaka nenda rudi. Kwamba vyombo vikubwa vya habari vikishamtangaza mshindi wa Urais, basi, aliyeshindwa huinua simu kumpigia mshindi na kumpongeza.
Kisha mshindwa huongea na wanahabari na kusema kuwa nimempigia simu mshindi kumpongeza.
Aliyeshinda naye hutoka hadharani na kuongea na wanahabari, kuupokea ushindi na kuwaambia kuwa mshindwa amenipigia kunipongeza.
Naye mshindi atampongeza mshindwa kwa uungwana wake na hata kuongeza mengine mazuri ya mshindwa.
Huo ndio utamaduni uliozoeleka wa demokrasia ya Marekani. Ni kama kuvunja mwiko fulani kwenda kinyume na utamaduni huo.
Kwanini Trump mara hii amevunja mwiko?
Jibu:
Jambo hili limetuumiza vichwa wachambuzi kupata tafsiri yake. Maana, Trump alikuwa kwenye kucheza golf wakati taarifa za ushindi wa Joe Biden zilipomfikia.
Cha kwanza alichofanya ni kuukana ukweli kwa kuandika kwenye akaunti yake ya tweeter;
” Nimeshinda, kwa kishindo!”
Imeshangaza wengi, lakini, yumkini, kwa mtazamo wangu, Trump kwenye akili yake anataka kuendelea kuwagawa Wamarekani akiamini anajenga mtaji wa uchaguzi wa 2024, ambao, kimsingi ana haki ya kugombea.
Na kama si yeye, huenda anajenga mtaji kwa bintiye Ivanka kurudi 2024 kama mgombea akiwa na sapoti ya baba yake na mkwe wa Trump, Kushner.
Kama Trump kuna atakachovuna kwenye hili wakati utasema.