**************************************
Dar Salaam. Mashindano ya riadha na mbio za baiskeli ya kusheherekea Uhuru wa Tanzania yamepangwa kufanyika Desemba 9 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kampuni ya Uhuru Sports Agency Leena Kapadia alisema jana kuwa wanariadha wa kike na wa kiume watashindana kwenye mbio za nusu marathon (kilometa 21) ambapo waendesha baiskeli watashindana mbio za kilometa 42.
Kapadia alisema kuwa mbali ya mashindano hayo, pia kutakuwa na mashindano ya kilometa tano ( 5) ya kukimbia au kutembea ambayo ni maalum kwa watu wazima, vijana na watoto na mbio za kilometa 10.
Alisema kuwa usajili wa mashiriki katika mashindano hayo utaanza Novemba 15 na kamati yao kwa sasa inatafuta wadhamini kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo muhimu ambalo litakuwa la kwanza kufanyika nchini.
“Haya ni mashindano ya kwanza ya kusheherekea Uhuru wa Tanzania kwa kushirikisha wanariadha na waendesha baiskeli. Kampuni yetu imesajiliwa na Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) na kupata namba ya usajili ya NSC 83 na tunatarajia kufanya mbio zenye mvuto na ushindani mkubwa,” alisema Kapadia.
Alisema kuwa pia wanakusudia kuona viongozi mbalimbali, makampuni ya umma, binafsi, mabalozi, taasisi kushiriki katika mbio hizi.
“Mfano, mbio za kilometa tano ni maalum kwa viongozi mbalimbali, familia na watu mbalimbali, wote hawa wanatakiwa kusheherekea Uhuru wa nchi yetu, hivyo tunawaomba wanamichezo kujisajili kwa ajili ya kushiriki katika mashindano haya,” alisema.
Alisema kuwa wanatarajia wanamichezo wasiopungua 3,500 kushiriki katika mashindano hayo ambapo miongoni mwao ni wanariadha nyota wa ndani ya nchi.
Kapadia alisema kuwa mashindano hayo pia yana lengo la kuendeleza mchezo wa riadha na baiskeli hapa nchini. “Hii ni fursa ya wanamichezo kujipima uhwezo wao kabla ya kuwania nafasi ya kufuzu mashindano mbalimbali ya kimataifa,” alisema.