MGOMBEA wa ubunge katika Jimbo la Mkuranga kupitia Chama cha Mapinduzi ( CCM) Abdallah Ulega,amemhakikishia ushindi wa zaidi ya asilimia tisini katika jimbo hilo mgombea Urais kupitia chama hicho Dk John Magufuli kutokana na wananchi wa jimbo hilo kumkubali.
Akizungumza wakati wa kampeni zake za ” lala salama” jimboni humo, Ulega alisema kimsingi ushindi wa Dk Magufuli jimboni humo upo wazi na kwamba haoni mtu mwingine yoyote anayeweza kuthubutu kupata kura zaidi yake.
Alisema amefanya kampeni zake katika vijiji 120 vilivyomo jimboni humo huku katika kila kijiji anachopita wananchi wake wakidai kufurahishwa na uchapa kazi wa Rais Magufuli, jambo linalotoa mwanga ya kuwa ushindi wake katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho ni mweupe.
Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi alisema kitu kingine kinachompa nafasi nzuri ya ushindi Rais Magufuli ni utetezi wake kwa wanyonge wa taifa hili ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wakipoteza haki zao.
“Wana Mkuranga walisema ‘yes’ kwa Dk Magufuli, wanasubiri kesho ifike ili waende kutimiza adhma yao ya kumpigia kura za ndiyo Dk Magufuli ” alisema Ulega.
Aidha aliwataka wananchi wa jimbo hilo na watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura hapo kesho ili kutimiza wajibu wao kikatiba wa kuwachagu viongozi mbalimbali.