Mama Askofu, Janeth Ndabila akiomba kwenye maombi hayo.
Mzee Gerald Enock akiomba huku akililia amani ya nchi isipotee wakati huu wa mchakato wa kupiga kura.
Katibu wa kanisa hilo, Jane Magigita (kushoto) akiomba katika maombi hayo. Kulia n Muumini wa kanisa hilo, Mariam Luvanda..
MARAIS wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu , Masipika, mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Wazee pamoja na Viongozi wa dini wameombwa kwa busara na hekima walizo nazo kumshauri Rais Dkt. John Magufuli ili aweze kuivusha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.
Ombi hilo linetolewa Jumapili na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila wakati wa maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu kesho.
Akihubiri katika maombi hayo Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu mara nyingi unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuashiria uvunjivu wa amani na utulivu wa nchi yetu.
“Baba pekee tunaye mtegemea kutuvusha salama katika uchaguzi huu ni Rais wetu Dkt. John Magufuli ambaye kikatiba bado ni Rais licha ya kwamba kesho tutapiga ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.” alisema Ndabila.
Alisema katika chaguzi nyingi duniani zimekuwepo changamoto kadhaa na ndio maana akawaomba viongozi hao wastaafu kumshauri Rais Magufuli azidi kuwa imara ili atuvushe salama katika uchaguzi huu kama alivyotuvusha katika kipindi kigumu cha ugonjwa wa Covid 19 na ndio maana wao kama kanisa wamefanya maombi hayo ikiwa ni kukumbushana kuitunza amani kuanzia kesho siku ya kupiga kura na siku za kuhesabu kura hadi kumpata Rais, Wabunge na Madiwani.
“Kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa, viongozi wastaafu na makundi mengine kwa njia ya maombi ili viwe na busara ya kulinda amani pasipo kuharibu utulivu wa nchi uliopo.” alisema Ndabila.
Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuonesha kuilinda amani ya nchi katika kipindi chote cha kampeni licha ya kuwepo changamoto ndogo ndogo na akaviomba vyama hivyo viendelee kufanya hivyo na kesho.
Alisema jambo linalo mpa amani ya kupiga kura kesho kwa amani ni kila mgombea alipokuwa kwenye kampeni jinsi walivyokuwa wakimtangulinza Mungu kabla ya kuanza mikutano yao.
Ndabila alisema amani inapokosekana wa kulaumiwa ni viongozi wa dini kwa sababu ndiyo wenye wajibu wa kuhamasisha waumini wao kumuomba Mungu atuepushe na uvunjifu wa amani wakati wote.
“Wagombea wote ni watoto wa Mungu hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu,” alisema Ndabila.
Ndabila aliomba hekima iongoze Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki, hekima iviongeze vyama vya siasa, hekima iviongoze vyombo vya usalamau na tuazimie kuto watoa watanzania kafara na kupoteza maisha ya mtanzania hata mmoja.
“Niwasihi viongozi wenzangu wa kidini pamoja na maombi mengi tunayoendelea nayo tunajukumu la kuwaondolea hofu watanzania na kusimama kwenye nafasi zetu kama wapatanishi. Imeandikwa her wapatanishi (Mathayo 5:9) na Mungu atatujalia kwa maombi yetu na hekima zetu kwa kushirikiana na Rais wetu aliyepo sasa kuivusha Tanzania kwa amani na salama.” alisema Ndabila.
Katibu wa kanisa hilo, Jane Magigita aliwahimiza waumini wa kanisa hilo na wananchi waliokuwepo kwenye maombi hayo kujitokeza kesho kwenda kupiga kura ya kumchagua Rais, wabunge pamoja na madiwani na akawaomba watanzania kuombea uchaguzi huo ili Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaoliongoza vema Taifa letu la Tanzania.
“Kila muumini na mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura kesho ajitokeze na kadi yake akapige kura katika kituo alicho jiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi na ya kikatiba.” alisema Magigita.
Aidha Magigita alisisitiza umuhimi wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo wa kupiga kura ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni na kuondoka kuelekea kwenye majukumu mengine baada ya kupiga kura kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza.