WAWINDAJI, wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamepatiwa elimu ya kufahamu haki zao na kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka.
Mafunzo hayo yametolewa na waelimishaji jamii kupitia shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) kwa ufadhili wa shirika la haki za binadamu la Legal Services Facility (LSF).
Muelimishaji jamii wa CSP, Obeid Sarakikya akizungungumza wilayani Simanjiro alisema ili kukuza ushiriki wa kundi hilo kwenye uchaguzi wanapaswa kufahamu haki zao.
Sarakikya alisema wanapaswa kufahamu vituo vya kupigia kura vilivyopo karibu na makazi yao na kutohama kwenye eneo walipo hadi upigaji kura utakapomalizika.
Amesema wanapaswa kujua kikamilifu siku na muda wa kupiga kura ili tuunde wapange ratiba ya shughuli zao mapema kwani huwa wanalisha mifugo mbali na makazi yao.
“Mpiga kura anapiga kura kwenye kituo cha sheria alichosajiliwa na asiyeweza kupiga kura au kutojua kusoma au kuandika anaruhusiwa kwenda na msaidizi na haruhusiwi kumchagua mtendaji wa uchaguzi,” amesema.
Mwanasheria wa CSP, Eliakim Paul amesema utaratibu wa kupiga kura kwa kutegemea hali ya mazingira ya kila eneo na kupiga kura kituo alichosajiliwa.
Eliakim amesema mpiga kura anatakiwa kupiga kura kwa amani, utulivu, uhuru na bila kulazimishwa na kupata usaidizi pale wamapohitaji.
Amesema matarajio ya wananchi ni kuona sheria na taratibu zote zinafuatwa kabla, wakati na baada ya kupiga kura, ulinzi na amani unadumishwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Pia matarajio ya wananchi ni kuona wapiga kura wote wanahudumiwa kwa usawa bila upendeleo isipokuwa kwa wenye uhitaji maalumu,” amesema.