Rais Dkt. John Pombe Magufuli akishirikiana pamoja na
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni
rasmi) kufungua kitambaa kwenye jiwe la msingi, wakati wa ufunguzi wa
rasmi wa msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini
Dodoma.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameungana na viongozi
wengine kupokea dua iliyokuwa ikisomwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh
Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni rasmi) katika ufunguzi rasmi
wa msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini Dodoma. Rais Dkt. John Pombe Magufuli akishirikiana kukata utepe na
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally (aliyekuwa mgeni
rasmi) pamoja na viongozi wengine, wakati wa ufunguzi wa rasmi wa
msikiti wa Chamwino, uliofanyika leo Oktoba 25, 2020 jijini Dodoma.
************************************
RAIS Dk.John Magufuli ameshuhudia uzinduzi wa Msikiti uliojengwa Chamwino- Ikulu katika Jiji la Dodoma ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Akizungumza leo Oktoba 26,2020 baada ya kushuhudia uzinduzi wa msikiti huo ambapo mgeni rasmi alikuwa Muft wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zuberi, Dk.Magufuli amesema pamoja na Tanzania kuwa na makabila,dini na rangi tofauti wameendelea kuwa wamoja na ujenzi wa msikiti huo ni ishara ya umoja na mshikamano uliopo nchini.
Amefafanua kuwa sifa moja wapo ya nchi yetu ni umoja na mshikamano walionao, watanzania hawajitambulishi kwa dini zao,kabila zao wala ukanda wanaotoka bali wanajitambulisha kwa Utanzania wao.”Kuna nchi zimeingia katika mapigano kwasababu ya dini, wengine makabila lakini sisi tunaishi kwa umoja na wala hatubaguani.
“Hii ndio sababu unaweza kwenda katika familia moja ukakuta kuna Mkristo na Muislam, ni kawaida kukuta mume ni mchaga na mke ni mgogo, ni kawaida kukuta wazazi ni Waislamu na mtoto ni Mkristo.Inawezekana Tanzania tu, kwengine haiwezekani.Hata hivyo hiyo haikuwa bahati mbaya bali imetokana na jitihada zilizofanywa na waasisi wa Taifa hili,walifanya kazi ya kujenga umoja na mshikamano,”amesema Dk.Magufuli.
Amesema kwa kutambua hatuna udini nchini kwetu Agosti 23 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Kanisa Katoliki Immaulate lilipo Chamwino , aliamua kuendesha harambee kuchangia msikiti huo baada ya kuona uliopo ni mdogo na umechakaa, hivyo aliona inafaa ujengwe mwingine.
“Waumini wengi waliokuwa Kanisani walitoa michango yao wakiongozwa na Baba Askofu na waumini wengine pamoja na wadau mbalimbali walishiriki kuchanga fedha na kupatikana Sh.milioni 319.3 zilizotumika kujenga msikiti huu.
“Nawashukuru wote waliochangia ujenzi wa msikiti huu, kwa yoyote aliyechangia msikiti huo asione amepoteza bali amefanya jambo lenye ujira mkubwa kwa Mungu na Koraani inasema msikiti ni nyumba ya ibada, kulitaja na kulinyanyua jina la Mwenzi Mungu, hivyo nawapongeza wote walioshiriki ujenzi wa msikiti huu.
“Msikiti huu ukatujenge pamoja kama ndugu, msikiti ukaendelee kuwaweka watanzania pamoja, msikiti huu ukatumike kumtanguliza Mungu wakati wote, msikiti ukatoe mafunzo yatakayojenga umoja wa watanzania, msikiti huu ukajenge umoja wa kweli ndani ya watanzania wote,”amesema Dk.Magufuli.
Aidha amesema watanzania wasikubali kuvuruga umoja na mshikamano, amani iliyopo hatuna budi kuitunzwa huku akitumia nafasi hiyo kuwambia Muft Sheik Zuberi zimebaki siku mbili tukapige kura na yeye mimi ni mgombea, hivyo watnzania watumie kuamua mazuri, kujenga umoja.”Tusisahau kwenda kupiga kura, tupige kura kwa utashi wa mioyo yetu, kwa mimi mwana CCM nitafurahi kama mtachagua madiwani wa CCM, wabunge wa CCM na mimi kwani ni wa CCM.”
Pia Dk.Magufuli amesema anamshukuru Muft kwa kukubali kuitwa kwa jina lake, Muft atakumbukwa kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika nchi hii, kwamba aliwahi kuwepo Muft Mkuu ambaye aliujenga umoja wa watanzania, narudia nawashukuru wajenzi
Amesisitiza “Muft Mkuu wewe ni wa pekee sana, ni mtu mpole, mwenye kujishusha na mpenda umoja, katika kipindi chako umejenga umoja, kwa Waislamu na wasio Waislamu, umejenga umoja wa watanzania, hivyo umewaenzi waasisi wa taifa hili kwa vitendo nalisema hili kwa dhati.”
Kuhusu ujenzi wa msikiti huo amesema anawashukuru masheikh, maaskofu, wachungaji wa dini na wananchi wote na hana cha kusema, kwani ujenzi wa msikiti huo ni ishara ya kipekee sio hapa nchini tu bali na duniani kote, huo ni upendo wa ajabu.
Dk.Magufuli amesema ujenzi wa msikiti huo umekamilika na kiasi cha fedha ambacho kimebakia katika ujenzi huo Sh.milioni 1.33 ni vema sasa ukaanza mchango mwingine kwa ajili ya kujenga nyumba ya ibada ya ibada ya Wasabato.”Tulianza na sasa Kanisa wanaosali Jumapili, tumefuata wanaosali Ijumaa na sasa tuanze safari ya kuanza kujenga nyumba ya ibada wanaosali Jumamosi.
“Kama nitaendelea kuwa Chamwino basi tutaendelea kujenga nyumba za ibada ya madhehebu yote, eneo hili ambalo linazunguka Ikulu nitafurahi kama litakuwa na nyumba nyingi za ibada ambazo zimezunguka ili watu wawe wanapata upako”.
Awali Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Muft Sheikh Aboubakar Zuber amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa ukarimu mkubwa alioufanya kwa Waislamu kwa kushawishi na kutengeneza utaratibu wa kupatikana msikiti wenye hadhi baada ya ule uliopo kuonekana hauna hadhi.
“Nakumbuka uliwasiliana na mimi kuhusu kuujenga msikiti huu, umekuwa ukiwapa heshima viongozi wa dini, umekuwa ukiwapa nafasi viongozi wa dini na umekuwa ukimpa kipaumbele Mungu, umekuwa ukijinyenyekeza mbele za Mungu,
“Kwa kasi kubwa ambayo umefanya ya kukusanya nguvu kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamechangia baada ya kuwahimiza kuchangia, waislamu na Wakristo wamechangia, Kanisa limechangia Kanisa limechangia, na watu wasipate tabu, jamani elimu ndogo udhia, Mtume Muhamad alipokea zawadi kwa wasio waislamu, sio vibaya kupokea zawadi kutoka kwa asiye Muislamu,”amesema Muft Mkuu.
Amesema wanalazimika kumshukuru Rais Magufuli kwa jambo kubw ambalo amelifanya na ameonesha mapenzi makubwa kwa wananchi wake, hivyo amempongeza kwa ujasiri wake hadi leo hii msikiti huu unapatikana.”Kunifanya mimi nitajike kwenye msikiti huu ni tukio kubwa lingine, ni mahaba makubwa, nikwambie tu tumefurahishwa na jambo hili na Waislamu tunakushukuru kwani umefanya mengi kwetu.
“Leo tunakabidhiwa Msikiti wa Chamwino …kabla ya hapo ulituombea msikiti mkubwa kabisa wa kimataifa uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, msikiti mkubwa mzuri na wenye hadhi.Umetuondoa aibu kutokana na kazi hii ya kutujengea msikiti, hivyo hatukushangwaza na ujenzi wa msikiti huu.
“Pia tunakushukuru kwa kufanikisha kurudishwa kwa mali za Waislamu ambazo zimepotea au kubabaishwa, tumefurahi sana katika hilo.Mtume anasema anayekufanyieni wema mlipeni, na kama hakuna cha kumlipa muombeni Mungu, namuomba Mwenyezi Mungu akupe maisha ya heri na afya njema wewe na familia yako na wasaidizi wako, na akufurahishe kama unavyowafurahisha waja wake,
“Tunamuomba Mungu atuvushe salama na uchaguzi mkuu, atulinde kabla na baada ya uchaguzi maana kuna maisha baada ya uchaguzi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kufika kwenye vituo vya kupia kura siku ya uchaguzi, atupe umakini na aturuzuku jicho la ndani tuwe na uchaguzi wenye radhi zake, nchi yetu aifanye iendelee kuwa kisiwa cha amani”.