************************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAPIGA kura wa Jimbo la Dodoma mjini wametakiwa kutumia haki yao ya kikatiba kwenda kupiga kura na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge na Madiwani bila wasiwasi.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, Wakili Msekeni Mkufya alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Wakili Mkufya alisema “wananchi ambao ni wapiga kura wa Jimbo la Dodoma mjini msiwe na wasiwasi wowote kwenda kupiga kura siku ya tarehe 28 Oktoba, 2020. Tumieni haki yenu ya kisheria kujitokeza kupiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge na Madiwani. Kama Msimamizi niliyepewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huu mwaka 2020, nawahakikishia Dodoma ni shwari na mazingira yanaruhusu kufanya hivyo. Vituo vitakuwa wazi kwa muda uliopangwa kuwaruhusu kupiga kura kwa mujibu wa sheria.
Aidha, mtu atapiga kura mahali alipojiandikisha na anatakiwa kwenda na kadi yake ya kupigia kura. Daftari limehakikiwa, ikitokea akapata shida ya kuona jina lake yupo karani na msimamizi wa kituo kutoa msaada huo, aliongeza.
Alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapiga kura. Hata kwa wale ambao hawaoni, zipo karatasi za nukta nundu kwa ajili yao, aliongeza. “Kwa wale wenye mahitaji maalum, Tume imetoa muongozo mtu huyo anaweza kuja na mtu anayemuamini kumsaidia. Tume imetengeneza mazingira mazuri hata katika vituo vya kupigia kura ile sehemu ya kupigia kura ya faragha imetengenezwa kwa muundo unaomruhusu mtu mwenye ulemavu kupiga kura na mtu siye na ulemavu kupiga kura kwa usawa” alisema Wakili Mkufya.
Jimbo la Dodoma mjini ni miongoni mwa majimbo makubwa likiwa na vituo vya kupigia kura 911, katika kata 41, likiwa na jumla ya wapiga kura 335,324.