NA EMMANUEL MBATILO
Mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Magufuli, ameendelea kuweka historia ya kutokamatika baada ya ripoti ya utafiti mwingine kuonyesha kuwa atawashinda wapinzani wake kwa kishindo katika Mikoa yote nchini.
Tangu kuanza kwa joto la uchaguzi wa mwaka huu, huo ni utafiti wa tatu unaotabiri ushindi wa Dkt. Magufuli, wakati tafiti mbili za awali zikijumuisha ushindi wake kitaifa kwa maana Bara na Zanzibar.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Taasisi ya Utafiti ya Gharus Technology ya nchini Ghana,Bi.Elena Riazanava, alisema utafiti huo umefanywa katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni hadi mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu.
Bi.Elena, alisema utafiti huo pia umehusisha maoni ya watu 48,239 wenye umri wa zaidi ya miaka 18, huku wanawake wakiwa asilimia 58 na asilimia 42 ni wanaume.
Alisema utafiti huo unaonyesha kuwa kwa upande wa Unguja, Zanzibar Dkt. Magufuli, atashinda kwa asilimia 84, Tundu Lissu wa Chama cha CHADEMA, atachaguliwa kwa asilimia 14 huku wagombea wengine wakipata asilimia mbili.
Alisema kwa upande wa Pemba, Zanzibar utafiti huo unaonyesha kuwa Dkt. Magufuli, atashinda kwa asilimia 55 akifuatiwa na Lissu atakayepata asilimia 43 na wagombea wengine wakiambulia asilimia mbili.
Elena, alisema katika mikoa ya bara, mkoani Simiyu, Dkt. Magufuli, ataongoza kwa asilimia 90, Lissu ataambulia asilimia nane na wagombea wengine wakipata asilimia mbili.
Alisema mkoani Moshi Dkt. Magufuli, ataongoza kwa asilimia 68, Lissu akitabiriwa kupata asilimia 30 na wagombea wengine wakiambulia asilimia mbili.
Kadhalika alisema kwa mujibu wa utafiti huo, mkoa wa Mwanza, Dkt. Magufuli, ataongoza kwa asilimia 77, Lissu atapata asilimia 20 na wengine wakiambulia asilimia tatu, huku mkoa wa Dodoma Dkt. Magufuli, akishinda kwa asilimia 86, Lissu asilimia 12 na wengine wakidaiwa kupata asilimia mbili.
Bi.Elena alifafanua kuwa utafiti huo, unaonyesha jijini Dar es Salaam Dkt. Magufuli, atashinda kwa asilimia 72, Lissu asilimia 27 na wagombea wengine asilimia moja na mkoa wa Arusha Dk. Magufuli, atapata ushindi wa asilimia 67, Lissu, 31 na asilimia mbili kwa wagombea wengine.
Kwa mujibu wa Bi.Elena, tafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 86 ya wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watamchagua Dkt. Magufuli, huku asilimia 12, watamchagua Tundu Lissu, asilimia moja watamchagua mgombea wa ACT Wazalendo, Benard Membe idadi ambayo watapata wagombea wengine pia.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, asilimia 72 ya wanawake watamchagua Dkt. Hussein Ali Mwinyi, asilimia 27 watamchagua Maalim Seif Sharrif Hamad wa ACT Wazalendo na wengine wataambulia asimilia moja.
Mchanganuo wa washiriki wa utafiti huo unaonyesha kuwa wanawake ni 27,979 na wanaume ni 20,260 na kati yao asilimia 95 watapiga kura.
TAFITI ZILIZOTANGULIA
Utafiti wa Asasi ya Trends Dynamiques Consulting Ltd ya nchini Kenya, ulionyesha kuwa kwa upande wa bara Dkt. Magufuli, atashinda kwa asilimia 80, Lissu atapata asilimia 18 huku vyama vingine vikiambulia asilimia mbili.
Pia utafiti huo ulionyesha kuwa upande wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi, atashinda kwa asilimia 67, Maalim Seif, akikadiriwa kupata asilimia 30 na vyama vingine asilimia tatu.
Pia utafiti mwingine wa Asasi ya Kiraia ya RhemaSoft ya nchini Ghana, ulionyesha kuwa katika uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli, atashinda kwa asilimia 82, huku wapinzani wake akiwemo mgombea wa CHADEMA, Tundu Lissu akikadiriwa kupata asilimia 16, Benard Membe wa ACT Wazalendo, asilimia moja kama ambavyo vyama vingine vya upinzani vitapata.
Utafiti huo pia unaonyesha Mgomea wa Urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Mwinyi atamshinda mpinzani wake kwa kupata ailimia 69, huku mpinzani huyo wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Shafiff Hamad, akikadiriwa kupata asilimia 29 na vyama vingine asilimia mbili.