………………………………………………………………………………….
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wana Mtwara wawe makini kuamua wanataka kiongozi wa aina gani kwani zimebakia siku saba tu kabla ya uchaguzi mkuu.
“Zimebaki siku saba tu, ndugu zangu kabla ya siku ya uchaguzi. Lazima tuwe makini na tutafakari ni aina gani ya kiongozi tunamtaka,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Oktoba 20, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kitangari, wilayani Newala kwenye mkutano uliofanyika kwenye stendi kuu ya Newala.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mtwara kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Newala Vijijini, Bi. Maimuna Mtanda na mgombea udiwani wa kata ya Kitangari, Bw. Mfaume Ladda.
Amesema wananchi wanapaswa kuamua aina ya kiongozi wa kumchagua ili aweze kuleta maendeleo ya haraka. “Maendeleo hayana chama sababu tukijenga shule watasoma watoto wetu wote. Kwa hiyo, nawaomba sana tumchague Dkt. Magufuli ili aje aendeleze mazuri aliyoyaanzisha.”
Kuhusu uboreshwaji wa miundombinu, Mheshimiwa Majaliwa alisema upanuzi wa bandari ya Mtwara unaendelea ambapo sh. bilioni 170 zilitolewa na Serikali ili ujenzi wa kitako kikubwa cha kuweza kuweka mizigo na magari zaidi ya 600 ufanyike.
“Vilevile sh. bilioni 50 zimetolewa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara ili uweze kupokea moja kwa moja ndege kubwa kutoka Ulaya bila kulazimika kutua kwanza Dar es Salaam.”
Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 89 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 210 ambayo itaunganisha wilaya nne na itaanzia Mtwara Vijijini – Nanyamba – Newala – Masasi.
Kuhusu zao la korosho, Mheshimiwa Majaliwa alisema mfumo wa mnada ulisaidia bei ya korosho ipande na kufikia sh.4,000/- lakini msimu uliopita bei ilizorota kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.
“Wanunuzi wa ndani walipanga kununua korosho kwa sh. 1,800/- lakini Mheshimiwa Rais aliamua kutoa sh. bilioni 900 ili zitumike kulipia ununuzi wa korosho za wakulima.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye awali alisimamishwa na wananchi wa kata ya Mkwiti, alisema Serikali imetoa sh. milioni 600 kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Mtama hadi Tandahimba kupitia Mkwiti ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Mtama hadi Tandahimba kutasaidia kuboresha biashara na usafiri baina ya maeneo hayo na Jiji la Dar es Salaam.”
Pia alimuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, na kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Tandahimba kwa tiketi ya CCM, Bw. Katani Ahmad Katani na mgombea udiwani wa kata ya Mkwiti, Bw. Ismail Iddi Said.