…………………………………………………………………
Na Masanja Mabula –Pemba.
ZAIDI ya watu 57 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana na vurugu zilizotokea oktoba 16 na kusababisba wanachama saba wa chama cha Mapinduzi kujeruhiwa.
Majeruhi hao saba akiwemo mama mjamzito inasemekana walipigwa na kitu chenye ncha kali huku utumbo wa mmoja wa majeruhi hao Khatib Said Khatib (43) ukitoka nje.
Akizungumza katika wodi wa wagonjwa ambako anapatiwa matibabu, Raya Khamis Hamad (24)alisema alipigwa na watu hao wakati akijaribu kumkoa baba yake mzazi baada ya kumuona anashambuliwa na kundi la watu.
“Nilipigwa wakati najaribu kumusaidia baba yangu ambaye alikuwa ameangushwa na watu ambao hata hivyo sijawafahamu majina yao lakini nikiwaona sura nazifahamu”alifahamisha.
Naye Khamis Hamad Haji (70) alisema vurugu hizo zilianza majira ya saa kumi na mbili nusu jioni wakati watu hao wakitoka kwenye mkutano wa Kampeni.
“Mimi walinikuta nimekaa nyumbani kwangu na kuanza kunishambulia , sikumbuki kuwa na ugomvi na mtu , nilipigwa jiwe tumboni na kwa kweli nimeumia sana”alieleza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba , Kamishna Msaidizi Juma Sadi Khamis alisema watuhumiwa hao wote ni wakaazi wa shehia ya Shumba ya Mjini Wilaya ya Micheweni.
Kamanda Sadi alisema pamoja na kuwakamata watu hao , bado Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
“Tunawashikilia watu 57 kwa tuhuma za kuhusika na vurugu zilizotokea katika kijiji cha Kwale Shehia ya Manjezi wilaya ya Micheweni zilizosababisha watu saba kulazwa katika Hospitali ya Micheweni”alisema.
Alifahamisha kwamba katika shehia ya Shumba ya Mjini wanaume wamekamimbia a inadaiwa kwamba wamekimbilia Shimoni nchini Kenya na waliobaki ni watoto na wanawake.
“Askari wetu wanaendelea kuwatafuta wahusika ambapo inasemekana kwamba wamekimbia nchini Kenya, lakini watambue kwamba sheria haikimbiwi hivyo ni bora warudi makwao”alisisitiza.
Waliojeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Micheweni ni pamoja Khamis Hamad Haji (70), Yassir Hamad Abdalla (18), Abdalla Khamis Mbwana (30),Juma Khatib Rajab (36),Hassan Khamis Hamad (23),Khatib Said Khatib (43) na Raya Khamis Hamad (24).
Daktari wa Zamu katika Hospitali ya Micheweni Dkr Yahya Faki Khamis alisema mama mjazimto wamemfanyia uchunguzi na kubaini kwamna hali yake pamoja na kiumbe tumboni wako vizuri.
“Tumemfanyia uchunguzi , Raya Khamis Hamad na tumebaini kwamba hali yake iko vizuri yeye pamoja na kiumbe tumboni, lakini bado yuko chini ya ungalizi wa kitaalamu”alisema.
Watu wanadaiwa kuhusika na vurugu hizo ni wafuasi wa Chama Cha ACT Wazalendo ambao kwa sasa asilimia kubwa wamehama makazi yao.