Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yaliyofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Boniphance Luhende ,akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yaliyofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Washiriki wa mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine,yaliyofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
……………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mawakili wa Serikali wametakiwa kuhakikisha wanafanya kwa ufasaha namna ya uandaaji Hati za madai, Maelezo ya Mashahidi, stadi za utetezi, na viapo vya maombi.
Kauli hiyo imetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata,wakati wa kuhitimisha mafunzo ya semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Mawakili wa serikali iliyojumuisha Mawakili kutoka mikoa mbalimbali jijini Dodoma
Aidha Wakili Malata amesema kuwa mawakili hao wanatakiwa kutumia kikamilifu mafunzo waliopata ili kwenda kukabiliana na kesi za rushwa ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika jamii.
“Kama inavyofahamika rushwa iko kila sehemu na kumekuwa na kesi za aina mbalimbali za rushwa katika vitengo tofauti hivyo nendeni mkafanyie kazi hilo” ameagiza Wakili Malata.
Wakili Malata amesema kuwa wanakila sababu ya kujiamini wanaweza kwa sababu wamejifunza vitu vya msingi ambavyo vinatumika katika kesi za kila siku .
Hata hivyo amewataka wakatekeleze kwa vitendo mafunzo waliyopatiwa ili kusaidia jamii na janga la rushwa nchini kwa kuwajibika kwa kufata sheria kanuni na taratibu za kazi yao.
“Nawaagiza kuzingatia maadili na miiko ya kazi yenu naamini wote mtakuwa mnajua wajibu wenu, “amesisitiza Wakili Malata.
Hivyo wakili Malata amesema kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni kwenda kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanaitendea haki taaluma hiyo ambayo ni muhimu sana katika jamii.