Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi kushoto na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar Mhe. Issa Haji Gafu wakitia saini Hati za makubaliano ya kuondoa Hoja 5 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ikiwemo ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya Kimataifa na Kikanda, Hafla iliyoshudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhun Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi iliyofanyika leo Octoba 17,2020 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam. Katibu Mkuu Kiongozi Bara Dkt. Alan Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee wakibadilishana Hati za makubaliano ya kuondoa Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi kuhusu uandaaji Vikao vya pamoja muda mfupi baada ya kusaini Hati hizo katika Hafla iliyoshudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhun Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi leo Octoba 17,2020 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Waziri wa Biashara Viwanda na Uwekezaji Mhe. Inocent Bachungwa kushoto na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Amina Salum Ali wakibadilishana Hati za makubaliano ya kuondoa Baadhi ya Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi kuhusu Biashara muda mfupi baada ya kusaini Hati hizo katika Hafla iliyoshudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhun Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi leo Octoba 17,2020 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihitubia Taifa kwa njia ya Televisheni na Redio kwenye kikao cha Utiaji saini Hati za makubaliano ya kuondoa Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi, ambapo Hoja 5 zimeondolewa ikiwemo ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya Kimataifa na Kikanda na Biashara, Hafla hiyo imefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam.
************************************
Na.Beatrice Sanga & Lilian Shembilu
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zimetia saini hati za makubaliano kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ambazo ni ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda, Ushiriki wa Zanzibar katika jumuiya ya Afrika Mashariki, gharama za kushusha mizigo bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 17 Oktoba, 2020 katika ukumbi wa mikutano Ikulu- Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali waserikali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mgombea urais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi pamoja na Wanasheria Wakuu wa Serikali wa pande zote mbili za Muungano.
Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa Serikali inazifanyia kazi hoja zote zitakazoletwa na mpaka sasa hoja tano (5) zimeshapatiwa ufumbuzi na kusainiwa ambapo hoja hizo zitaenda kuhamasisha uwajibikaji, kudumisha ushirikiano kati ya pande zote mbili za Muungano pamoja na kupelekea maendeleo yatakayo wezesha kukua kwa uchumi.
“Kusainiwa kwa hati hizi leo bila shaka kutaongeza ari na hamasa kwa pande mbili za Muungano, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika kuzidisha ushirikiano ambao unapelekea kwenye kuulinda na kuudumisha Muungano wetu.” Amesema Mama, Samia Suluhu Hassan.
Aidha, ameongeza kuwa, katika Muungano wa watu changamoto haziwezi kuisha na kuwepo kwake haimaanishi kuwa Muungano unatatizo au hauna umuhimu ila ni kuimarisha sera na kutafuta ufumbuzi utakao kuwa na manufaa kwa Watanzania na Wazanzibar.
Mama Samia alibainisha kuwa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zitawezesha utaratibu mzuri wa namna ya kuendesha vikao, kuongeza uhuru wa kutumia rasilimali kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Pia kutapelekea wafanyabiashara wa pande zote mbili kufanya biashara zao bila vikwazo hali itakayoipa Zanzibar fursa zaidi katika masuala ya Kimataifa na Kikanda, kwa lengo la kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kuwa kusainiwa kwa hati za makubaliano zilizolenga kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi inatosha kuelezea namna SMT na SMZ zilivyojikita katika kutatua changamoto za Muungano kwa maslahi mapana ya wananchi na aliishukuru sekretarieti ambayo imewezesha hatua hiyo.
“Ni imani yangu kuwa Wizara zote za SMT na SMZ, zitaendelea kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti na kuhakikisha maagizo yanayotolewa na vikao vya pamoja yanafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa”, Amesema Kassim Majaliwa.
Hatahivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amewashukuru wajumbe wote wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano ambayo kwa kiasi kikubwa yanaenda kupelekea maendeleo makubwa kwa wananchi wa pande zote na ameeleza kuwa hoja nyingine sita (6) ambazo tayari mpaka sasa zimeshapatiwa ufumbuzi na zinasubiri kupata ridhaa ya kikao cha kamati ya SMT na SMZ.
“Pamoja na kwamba leo tutaondoa hoja tano (5) katika orodha ya hoja za Muungano, naomba kuchukua fursa hii kueleza kuwa, hoja nyingine sita (6) zimepatiwa ufumbuzi zinasubiri kupata ridhaa ya Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ kama ilivyoainishwa katika Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ Aya ya 2.2 (b).” amesema Mhe. Zungu.