Home Makala NJOMBE!!!! KESHO NJEMA INAJENGWA NA LISHE BORA ENDELEVU

NJOMBE!!!! KESHO NJEMA INAJENGWA NA LISHE BORA ENDELEVU

0

Na Judith Mhina-Maelezo

Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu maneno haya yametanda katika kona zote za Mkoa wa Njombe unaoadhimisha Kitaifa Siku ya Chakula Duniani kuanzia tarehe 10 mpaka 16, Oktoba. 2020 yenye kauli mbiu ya “Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu”.

Maadhimisho haya hayakwenda Njombe kwa bahati mbaya bali ni kutokana na changamoto kubwa ya utapiamlo na udumavu uliokithiri katika Mkoa wa Njombe na kuongoza kufikia asilimia 53.6.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma hivi karibuni Naibu Waziri wa Kilimo , Omary Mgunda alitaja Mikoa inayokabiliwa na changamoto ya utapiamlo na huku ikiwa kinara katika uzalishaji wa chakula ni Mkoa wa Njombe, Iringa, Kigoma, Ruvuma, Rukwa na Songwe.

Mgunda alisema Mikoa hiyo inazalisha chakula kwa viwango vikubwa, lakini ndio inaongoza kwa kuwa na udummavu. Hivyo, Serikali imejipanga kutokomeza tatizo hilo kwa kutoa elimu juu ya matumizi ya vyakula vya kuongeza lishe kwa wingi

Kufuatia hali hyo Wizara ya Kilimo imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa masuala ya lishe ili kuondoa tatizo hilo nchini.

Elimu ya lishe ndio mpango uliokadiriwa na kupangwa kuanzia ngazi ya Taifa mpaka Kata, ambapo Mkoa wa Njombe umejipanga kutoa elimu ya lishe kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka Kijiji.

Aidha, kutokana na uzalishaji mzuri wa vyakula vya aina mbalimbali kama mahindi , viazi mviringo, maziwa, aina mbalimbali za mboga na matunda kama vile maparachichi,  wazazi na walezi  wanaelimishwa kwa kiasi kikubwa jinsi ya kuandaa chakula kinachowafaa watoto, wajawazito, vijana na wazee ili kulinda afya zao.

Akiongea na hadhara ya maandalizi ya Siku ya Chakula Duniani Mkuu wa Mkoa wa Njombe Marwa Rubirya alisema kuwa ni lazima mila na desturi zinazopotosha jamii katika suala zima la lishe  ziachwe mara moja ili kuzalisha Taifa lililo bora na imara kwa sasa na hapo baadaye.

Ameongeza kusema kuwa maonyesho yanafanyika katika viwanja vya Mji Mwema ambapo takriban washiriki 200 wana mabanda ambayo yanaonesha mazao mbalimbali muhimu katika kupunguza au kuondoa kabisa utapiamlo na udumavu.

Pia, amesisitiza matumizi ya teknolojia zilizo sahihi katika kuhakikisha uzalishaji chakula kilicho bora na salama kwa afya ya walaji kwa kuhakikisha virutubisho vya  kinachozalishwa unabaki pale pale bila kuathirika.

Hali Halisi ya Udumavu Nchini

Akionyesha hali halisi ya udumavu na utapiamlo katika mikoa hiyo Mgunda alisema “Serikali imejipanga kuhakikisha mikoa hiyo inaondokana na udumavu hivyo, kupitia Siku ya Chakula Duniani wataalamu watatoa elimu jinsi ya matumizi ya vyakula vya lishe, wakati Mkoa wa Njombe una udumavu kwa asilimia 53.6 huku ukizalisha chakula tani 446,491”, alisema Mgunda.

Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Rukwa una asilimia 47.9 ya udumavu wakati unazalisha chakula tani 943,002, huku kiwango cha utoshelevu kikiwa ni asilimia 230.

“Mkoa wa Iringa una asilimia 47.1 ya udumavu wakati unazalisha tani za chakula 470,750 kiwango cha utoshelevu ni asilimia 161, Songwe ina asilimia 43.3. wakati uzalishaji chakula ni tani 805,545 kiwango cha uteshelezi ni asilimia 210” alisema Mgunda.

Aliongeza na kusema kuwa, Mkoa wa Kigoma una asilimia 42.3 ya udumavu huku ukizalisha tani 1,158, 214, kiwango cha utoshelezi ni 165 na Ruvuma una asilimia 41.0 ya udumavu na unazalisha tani 1,251,511 kiwango cha utoshelezi ni 237.

Kwa Nini Utapiamlo Njombe

Hali hii ya utapiamlo ambao umeleta udumavu wa asilimia 53.6 umetokana na wazazi, walezi wa Kaya mbalimbali na walimu kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi na kutotilia mkazo suala la kuangalia familia zao pamoja na walimu kufundisha stadi za maisha.

Katika hatua nyingine, Mgunda alisema wiki ya Chakula, iliyozinduliwa Oktoba 10, mwaka huu yenye  madhumuni ya kuwezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza teknolojia sahihi za kuongeza uzalishaji na mbinu za kutokomeza njaa.

Amesema mpango huo umeanza mwaka 2020/21 ikiwa ni sehemu ya programu ya kuendeleza sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP 11) ambao unaainisha majukumu mbalimbali ya wadau katika kuchangia kupunguza lishe duni nchini.

Vilevile, Wizara inaendelea kuboresha miongozo mbalimbali ya kutoa elimu namna ya kuzalisha, kuhifadhi na kutumia mazao ya mikunde kama vile soya, choroko, mbaazi na dengu ambayo yana viini lishe aina ya protein.

Jitihada za Kukabiliana na Utapiamlo Njombe

Uzinduzi wa Mpango Kielelezo wa Viwanda umezinduliwa na  Katibu Mkuu wa Wizara ya viwanda Profesa Riziki Shemdoe kupitia Mradi wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP 11) amesema “Hii ni programme iliyoandaliwa ili  kutusaidia sisi kuwekeza katika miradi ya viwanda hivyo kuchakata products zinazotoka katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi”

Naye Profesa Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambaye ni Mtaalamu wa Lishe amesema “Lazima kutoa elimu kwa wakulima, wavuvi na wafugaji  ili kuwa na uhifadhi na uvunaji  sahihi kwa kuwa  asilimia 30 hupotea katika zoezi hilo na nguvu za wakulima zinapotea bure”.

Nayo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Uyole Mbeya, imegundua aina ya mbegu bora ya ulezi ambayo inazaa mara nne zaidi kwenye hekari moja ikilinganishwa na mbegu ya awali ambayo ilikuwa inazaa kilo 1,000 kwenye hekari moja, hayo yamesemwa na Dkt Tulole Bucheyeki Mkurugenzi TARI Uyole.

“Siku ya Chakula Duniani inasisitiza lishe bora na sisi TARI Uyole tumetengeneza aina tatu za ulezi ambazo ni U-15, P-224 na TARI FM-I zina uwezo wa kutoa mavuno tani 4.5 kwa hekta moja maana yake unaweza kupata magunia 18 kwa hekari moja ukiuza kwa bei ya elfu tatu unaweza kupata milioni hamsini na kuendelea na ukawa milionea ambapo unaweza kuzitumia kuanzisha kiwanda cha kusindika ulezi”.

Aidha, ameongeza kuwa,  ulezi huu una virutubisho vingi muhimu vinavyoweza kukabiliana na tatizo la utapiamlo kama vile protein kwa wingi, wanga, madini ya calcium, vitamin A na mafuta, virutubisho hivi ni muhimu kukabiliana na utapiamlo”

“Hivyo, ulezi unaweza kumtajirisha mkulima ambapo ni zao la asili la biashara , unaweza kulima ulezi na ukawa bosi kwa maana ya kuajiri wanajamii wanaokuzunguka, kwa hiyo basi tunatoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hii kwa kulima ulezi ili kutokomeza udumavu na utapiamlo pamoja na kushiriki kikamilifu kufanya biashara na kuongeza kipato”.

Mnamo tarehe 30 Oktoba, mwaka 2019 Sekretarieti ya Mkoa wa Njombe iliaadhimisha siku ya Afya na Lishe ya Kijiji katika Kata ya Mahongole, Halmashauri ya Mji Makambako na kutoa rai kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya lishe bora kwa ajili ya kukabiliana na utapiamlo na udumavu.

Afisa Lishe Mkoa wa Njombe, Bi. Betha Nyigu aliongea na wakazi wa kijiji cha Mahongole na kutoa wito kwa wanawake na wanaume kuzingatia afya ya mtoto ili kukabiliana na tatizo linalotokana na udumavu kwa watoto.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, Nyigu alisema kuwa katika mkoa wa Njombe hali ya udumavu imefikia asilimia 53.6 na kuufanya mkoa kuwa wa kwanza kitaifa.

“Lengo la kuja katika kijiji cha Mahongole kufanya maadhimisho haya ya siku ya Afya na Lishe ni kuangalia utekelezaji wa mkataba wa lishe katika ngazi ya jamii ambapo moja ya kiashiria kilichopo ni utekelezaji wa siku ya Afya na Lishe,” alisema  Nyingu.

Aidha Afisa Lishe huyo wa Mkoa wa Njombe alisema waliamua kuwafikia wananchi wa kijiji cha Mahongole kama muendelezo wa kutoa elimu ya lishe na kuona hali halisi. Pia, kwa lengo la kuzungumza na wakina mama na kina baba juu ya changamoto ya utapiamlo pamoja na udumavu ambao unakabili kijiji hicho kwa baadhi ya watoto.

Hapa Tanzania kiasi cha watoto 130 hupoteza maisha kila siku kutokana na kuosa lishe bora, lishe duni hudumaza ukuaji wa watoto kimwili na kiakili na hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na pia kupunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima.

Kiasi cha asilimia 42(zaidi ya milioni tatu) ya watoto wa Tanzania wa umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa kutokana na lishe duni kabla ya kuzaliwa . Udumavu ni wa kiwango cha juu sana katika sehemu nyingi Tanzania, ikiwa ni pamoja na Mikoa yenye uzalishaji mkubwa kama vile Njombe, Iringa, Kigoma, Songwe, Rukwa, Kagera hata Arusha.

Vilevile kiwango cha udumavu Tanzania ni zaidi au karibu sawa na asilimia 40 kwa watu wazima wote isipokuwa tu kwa wenye vipato vya juu wachache wanaokadiriwa kuwa takriban asilimia 20. Ushahidi huu unaashiria kwamba chanzo hasa cha udumavu ni zaidi ya upungufu wa chakula na umaskini wa familia. Mifano ya madhara ya kiafya kutokana na lishe duni ni pamoja na utapiamlo mkali , ambao kwa Zanzibar pekee asilimia 12 ya watoto wameathirika . Upungufu wa Vitamin A  ambao nao ni matokeo ya lishe dun hudhoofisha kinga mwilini na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo vya watoto.

Lishe bora kwa wasichana na wanawake wanaopata mlo kamili kabla na wakati wa ujauzito wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujifungua watoto wenye afya. Wanawake wanapaswa kupata chakula bora zaidi kilishe wakati wa ujauzito na kutofanya kazi ngumu hasa katika miezi mitatu ya mwisho kabla ya kujifungua. Kuhudhuria kliniki ya uzazi walau mara nne wakati wa ujauzito ni muhimu kwa ajili ya ufuatiliaji wa afya ya mama na ya mtoto ambaye hajazaliwa.

HAKIKA KESHO NJEMA INAJENGWA NA LISHE BORA ENDELEVU