Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi ndogo ya makao makuu Lumumba jijini Dar es salaam kuhusu Kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28 ,2020.
……………………………………………..
Na.John Bukuku,Dar es Salaam
Zikiwa zimesalia siku 10 kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu, Chama cha Mapinduzi(CCM),kimetoa tathmini ya kampeni zake huku kishindo cha kampeni za Mgombea urais wa CCM, Dk.John Magufuli zikielekezwa Mikoa sita kuanzia Pwani na kuhitimishwa Dodoma.
Mikoa mingine ambayo Magufuli atafanya kampeni ni Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara huku Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan akielekea Zanzibar na Morogoro na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa atakuwa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema kabla ya kampeni CCM ushindi wake haupungui asilimia 75 na kamati ya ushindi ilikuwa imejiwekea malengo ya kura za urais ni asilimia 90%, wabunge asilimia 75 na madiwani asilimia 80 huku urais Zanzibar asilimia 75.
“Tumekubaliana kila wanachama watatu wa CCM watuletee mtu mmoja, kutoka kwenye idadi ya wanachama wote milioni 17 wakifanya hivyo, tutapata kura za ziada milioni 5, ukijumlisha na milioni 17 unapata milioni 22, kwa idadi tu ya wana CCM wenyewe tuna ushindi wa 75%,”amesema
Amebainisha asilimia 89 ya mikutano yote aliyoifanya Magufuli ameifanya asubuhi na mikutano yote imekuwa inasheheni watu.
Kadhalika, Polepole amekemea kauli za kichochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
“Kumekuwa na kauli za uchochezi, mgombea urais wa chama cha Zitto kabwe kule Zanzibar aliwaambia wafuasi wake wachukue mapanga na mawe wawe tayari, leo tunavyozungumza wana CCM wamevamiwa na kupigwa na kuumizwa kule Pemba, leo tunavyozungumza hapa, kuna wana-CCM wamevamiwa, wakapigwa na kuumizwa Visiwani Pemba, hii ni siku moja baada ya mgombea Urais wa ACT-Wazalendo kusimamishwa kampeni kwa siku tano,”amesema.