……………………………………………………………………
Na John Walter-Babati
MGOMBEA udiwani kata ya Maisaka Mjini Babati kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Ramadhan Mungwe ameahidi kutatua mgogoro uliopo kati ya wananchi na Mwekezaji wa shamba la Tina Estate.
Mungwe alitoa ahadi hiyo wakati alipokutana na wananchi wa kijiji cha Kiongozi kata ya Maisaka kunadi sera zake ambapo pamoja na mambo mengine aligusia namna atakavyoimarisha mazingira bora ya ufanyaji wa biashara kwa kuanzisha soko la bidhaa katika eneo hilo.
Alisema kama wananchi wa Kiongozi wanapata shida kwenda mbali kununua bidhaa kwa sababu hawana soko hivyo akawataka wananchi kumchagua ili kupitia sera yake hiyo mtambuka awasaidie.
Alisema akipata nafasi ya kuwawakilisha wananchi katika baraza la Madiwani atashinikiza kuwepo kwa soko hilo na kuzungumza na Wamiliki wa shamba la Tina Estate na kukubalina ili kufikia muafaka katika shamba hilo.
Akizungumzia Miundo Mbinu ya barabara , amesema atahakikisha maeneo Korofi yote yanafanyiwa kazi katika kipindi cha uongozi wake.
“Mfano kumekuwa na barabara hapa Kiongozi iliwahi kuwa ya kiwango cha Moram, sijajua ni kwa nini haipandishwi kuwa ya kiwango cha lami wakati, hadi leo imebaki kuwa ya vumbi, mwisho wa siku watu watapata ugonjwa wa TB” alisema Mungwe
Kwa upande Mwingine Mungwe amewataka wanasiasa kutumia majukwaa vizuri kunadi sera za vyama vyao na sio kuwagawa wananchi kwa sababu ya itikadi za vyama vyao.
“Huwezi ukatuondolea Undugu kwa sababu ya Siasa, Ccm itabaki kuwa Ccm,Nccr Mageuzi itabaki kuwa kama ilivyo na Chadema hivyo hivyo” alisema