Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma kuhusu wananchi kuchukua tahadhari na njia za kuepuka na magonjwa ya Mlipuko katika kipindi hiki cha Mvua za Masika zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali.
………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
MGANGA Mkuu wa Serikali,Prof. Abel Makubi amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwakuzingatia suala la usafi kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo mbalimbali hapa nchini.
Prof.Makubi ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wananchi kuchukua tahadhari na njia za kuepuka magonjwa ya mlipuko katika kipindi cha mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo maeneo mbalimbali nchini.
Prof.Makubi amesema kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa kama ya kuhara ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu,kuhara damu na yale yanayoenezwa na Mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue endapo wanachi hawatazingatia kanuni za Afya na kuchukua tahadhari mapema.
“Wote tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa mioundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii inaweza kuhatarisha afya ya jamii na na kuongeza uwezekanio wakusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko,”amesema Prof.Makubi
Aidha amesema kwa sababu hiyo Wizara imeona bora kutoa taarifa na tahadhari kwa umma ili kuweza kuchukua tahadhari na kuelekeza njia za kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.
“Ili kuweza kuandika historia ya kutokomeza kabisa kipindupindu na magonjwa mengine hatuna budi kukumbushana na kuchukua tahadhari kwa kila mwanachi,Taasisi na viongozi wa ngazi zote ili kujikinga na kuzingatia kanuni za afya kwa kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalum kama waterguard kabla ya kuyatumia na kuhakikisha maji ya kunywa na yale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi,”alisistiza Prof.Makubi
Prof.Makubi aliendelea kufafanua ni vyema kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama,kutumia ipasavyo vyoo na kunawa mikono kwa maji safi yanayo tiririka na sabuni mara kwa mara kabla ya kula baada ya kutoka chooni,baada ya kumuhudumia mgonjwa pamoja na kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula.
Pia amewataka wananchi kuongeza usimamizi wa usafi wa ujumla na mikono katika maeneo ya mikusanyiko kama mashuleni,Vyuo na Masoko,kutotapisha vyoo au kutiririsha maji taka,kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu muda wote na kutumia ipasavyo vyandarua
Aidha, amewataka waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa,wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo lililo chini yao haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko.
Hata hivyo.Prof.Makubi amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wazee na Watoto hakujaripotiwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu hadi sasa.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti magonjwa haya ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao ulikoma Julai2019 na hii inatokana na jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na ushirikiano mzuri wa wanachi,”amesema .