*************************************
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba
huduma za kibenki zinazotolewa na benki na taasisi za fedha nchini
zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa wateja kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.
Hivyo, Benki Kuu inawataka wananchi kupuuza taarifa potofu zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba kuna maelekezo ya kusitisha huduma hizo muhimu katika kipindi cha uchaguzi.
Benki Kuu ya Tanzania, kama msimamizi wa benki na taasisi za fedha, haijatoa maelekezo yoyote ya kusitisha huduma za kibenki kwa wateja wa taasisi hizo. Wananchi wataendelea kupata huduma zote za kibenki kama kawaida wakati wote kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi.
Aidha, Benki Kuu inapenda kutoa onyo kwa mtu, watu au kikundi cha watu wenye dhamira ya kuupotosha umma na kusababisha taharuki katika jamii kwa kutoa taarifa za uongo. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, watu au kikundi chochote kitakachobainika kutoa taarifa potofu kwa umma.