Na Jovina Bujulu-MAELEZO)
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni chombo chenye mamlaka kisheria ya kuratibu na kusimamia Uchaguzi Mkuu na Chaguzi ndogo ambacho ambayo ilianzishwa rasmi Januari 13, 1993, chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
NEC katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya kuwa chombo kinachoaminika katika kusimamia uchaguzi Afrika huku kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, ugawaji wa majimbo na utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha demokrasia.
Pamoja na majukumu mengine ya NEC, pia inasimamia maadili ya uchaguzi ambayo ni makubaliano ya pamoja baina ya Vyama vya Siasa, Serikali pamoja na Tume yenyewe. Maadili haya hueleza mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa katika mchakato wa uchaguzi, wakati wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Aidha, maadili ya uchaguzi yanahusu kuheshimiana, kuzingatia ratiba ya kampeni, kuelimisha wanachama wa vyama katika misingi ya kuelewa sera za vyama husika, kutojenga chuki, kushirikiana na kutobeba silaha za aina yoyote katika mikutano ya kampeni.
Katika kutekeleza maadili haya, Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi ngazi ya Kata anatakiwa kutekeleza zoezi la kusimamia na kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya Tume kwa kuzingatia uwazi na uadilifu. Hivyo, Vyama vya Siasa vinawajibu wa kuzingatia Kanuni na Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ili kuepuka madhara yanayoweza kusababisha kuharibika kwa mchakato wa Uchaguzi.
Ili kuhakikisha maadili haya yanatekelezwa, Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi ngazi ya Kata anawajibu wa kuunda kamati za maadili katika ngazi ya Jimbo na Kata baada ya kupata maelekezo kutoka Tume na atatakiwa kuvitaarifu Vyama vya Siasa, Serikali na kuwasilisha majina ya wajumbe siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Kamati zitakazoundwa ni pamoja na Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa, na Kamati ya Maadili ya Rufaa, ambapo majukumu ya kamati hizo ni kusimamia na kushughulikia malalamiko yanayotokana na ukiukwaji wa maadili wakati wa kampeni za uchaguzi kuanzia hatua ya kuanza kampeni hadi kukamilika kwake.
Kila kamati itakuwa na mwenyekiti na wajumbe ambao watatokana na aina ya kamati, kwa mfano Kamati ya Maadili ya Kata itakuwa chini ya uenyekiti wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata na wajumbe ni mwanachama mmoja kutoka kila chama cha siasa chenye mgombea udiwani na mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na Katibu Tawala wa Wilaya.
Kwa upande wa Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, mwenyekiti wake atakuwa ni Msimamizi Msaidizi, ngazi ya Jimbo na wajumbe wake ni mwanachama mmoja kutoka kwenye chama cha siasa chenye mgombea wa ubunge na mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na Katibu Tawala wa Wilaya.
Kamati nyingine ni ya Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa ambayo Mwenyekiti wake ni mjumbe yoyote wa Tume atakayeteuliwa na Tume ambapo wajumbe watakuwa ni mwanachama mmoja kutoka kwenye chama cha siasa chenye mgombea wa kiti cha Rais na mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Fauka ya hayo, pia ipo kamati ya Maadili ya Rufaa ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye Chama cha Siasa chenye mgombea wa Kiti cha Rais na Mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa mwongozo wa elimu ya mpiga kura uliotolewa na NEC, umeainisha baadhi ya matukio ya ukiukwaji wa maadili kuwa ni pamoja na matumizi ya lugha za kashfa na matusi kwa wagombea na viongozi wa Vyama vya Siasa wakati wa kampeni, kuzidisha muda wa kampeni, kukiuka ratiba ya kampeni, maandamano ya wafuasi wa Vyama vya Siasa yasiyokuwa na kibali cha Jeshi la Polisi kabla na baada ya kampeni, wafuasi wa vyama kuharibu mabango ya wagombea wa vyama vingine, kubandika picha za wagombea juu ya picha za wagombea wengine, wafuasi wa vyama na wagombea kuingilia mikutano ya wagombea wa vyama vingine pamoja na kutoa kauli zisizoweza kuthibitishwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Kifungu cha 46 (1) , Sura ya 343 na Kifungu cha 53 (1) cha Sheria ya Uchaguzi yaSerikali za Mitaa, Sura ya 292. kipindi cha kampeni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hutangazwa na NEC ambapo kampeni zitaanza siku moja baada ya siku ya uteuzi na kumalizika siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.
Aidha, Kanuni ya 40 (1-5) na 41 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020 zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye ataratibu ratiba ya kampeni za Uchaguzi wa Kiti cha Rais na atavitaka Vyama vya Siasa vinavyoshiriki Uchaguzi wa Rais kuwasilisha ratiba za kampeni siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Hakika ratiba ni muongozo unaosaidia wagombea kutokuingiliana katika kampeni zao wakati wa kampeni, hivyo, mambo muhimu yakuzingatia wakati wa uandaaji wa ratiba zao ni pamoja na tarehe, muda, mkoa, wilaya na mahali ambapo mgombea atafanya kampeni zake na Mkurugenzi wa Uchaguzi akipokea mapendekezo ya ratiba za kampeni kutoka kwenye Vyama vya Siasa ataitisha mkutano kwa ajili ya kuratibu ratiba hizo.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 42 (1-5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, ratiba ya Kampeni za Uchaguzi wa Ubunge zitaratibiwa na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ambapo kila Chama cha Siasa au Mgombea atapaswa kabla ya kuanza kampeni kuandaa mapendekezo ya ratiba na kuiwasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Mratibu wa Kampeni za Udiwani kwa mujibu wa Kanuni ya 35 (1-5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2020 ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata, ambapo kila Chama cha Siasa au Mgombea atapaswa kabla ya kuanza Kampeni kuandaa mapendekezo ya ratiba ya kampeni na kuiwasilisha kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Uchaguzi utafanyika Oktoba 28, mwaka huu 2020 ni wa sita tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mnamo mwaka 1992 ambapo Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1995, ukifuatiwa na Uchaguzi wa Mkuu wa mwaka 2000, 2005, 2010 na 2015.