Na. Epifania Gustafu-MAELEZO
Mabalozi wapya wa Uingereza, Pakstani na Uswisi nchini wamefurahwa na mfumo wa kidemokrasia unaotumika nchini Tanzania kwa kuwa na mfumo huo unatoa nafasi wa kubadilishana madaraka kupitia chaguzi mbalimbali ikiwemo Uchaguzi Mkuu.
Wakizungumza Ikulu Jiini Dar es Saalam, wamesema kuwa wameridhishwa na mwenendo wa kampeni zinazoendelea sasa nchini na kuongeza kuwa hilo ni somo kwa mataifa mengine. Mabalozi hao David Cancar wa Uingereza, Muhammad Saleem wa Pakistan na Dider Chassot wa Uswisi wamesema hayo baada ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Rais John Pombe Magufuli.
Aidha Mabalozi hao wameongeza kuwa uhusiano baina ya nchi zao na Tanzania unaendelea kuimarika na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na ushirikiano katika mambo mbalimbali ya kimataifa ikiwemo utalii na uwekezaji.
Pia, Balozi wa Uingereza Cancar amesema anaridhishwa na hali ya kampeni ya uchaguzi inavyoendelea Tanzania na kwamba matumaini yake hali itakuwa nzuri hadi mwisho wa uchaguzi.
Tumezungumza na Rais Magufuli mambo mengi ya kuimarisha zaidi uhusiano wetu masuala ya uchumi,uwekezaji, fursa mbalimbali lakini pia, tumezungumzia uchaguzi ujao unaendelea vizuri na tunaamini utaenda hivyo na salama hadi mwisho kwa manufaa ya Watanzania wote. Alisema Balozi Cancar.
Balozi wa Uswisi Chassot amesema ameridhishwa na mfumo wa utawala wa unaolenga kubadilishana madaraka, amesema anaamini Uchaguzi Mkuu 2020, utafanyika katika mazingira ya amani kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya kuigwa duniani kote.
“Tumezungumza na Rais Magufuli masuala mbalimbali, sisi tunaomba demokrasia ya Tanzania ni nzuri hasa mfumo wa utawala wa kidemokrasia wa kubadilishana madaraka kwa njia ya amani, uchaguzi ujao tunaamini utakwenda vizuri na matumaini yetu utafanyika salama na kwa amani ni mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine” .Alifafanua Balozi Chassot
Akizungumzia uhusiano baina ya Uswisi na Tanzania, Balozi Chassot amesema anashukuru kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi yake nchini Tanzania, na ameeleza kuwa matumaini yake ni kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mataifa hayo.
Alitaja maeneo ya vipaumbele kuwa ni kusaidia fursa za ajira na ukuzaji kipato miongoni mwa Watanzania, kusaidia Serikali kuboresha sekta ya afya kuangalia utawala bora na kusaidia kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji wa viwanda vya kusindika mazao na vile vya kuchakata madini
“Tunaangalia kwenye maeneo ya kushindika ya viwanda mazoa na viwanda vya kuchenjua madini tujenge kitu ili mchango wetu na uhusiano wa kidiplomasia uendelee kuimarika na wananchi wakinufaika kwa uhusiano wetu”, alisema Balozi Chassot.
Katika kutekeleza ukuzaji uchumi hasa kwa kuwaangalia wakulima, upo mradi wakuzuia upotevu wa mazao baada ya kuvunwa unaogharamiwa na Uswizi, ambao wakulima wanapewa elimu ya jinsi ya kuvuna vizuri mazao na kuwa na usalama wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Uswisi inasaidia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuwajengea uwezo maafisa wa taasisi hiyo kwenye eneo la uchuguzi na urejeshwaji mali iliyopotea kwa njia ya rushwa
Vilevile Balozi huyo amezungumzia dhamira yake ya kuwashawishi, Waswizi kuwekeza nchini,Tanzania na kuangalia fursa ya kujenga viwanda ikiwemo kiwanda cha saa.
Balozi Chassot amesema Uswisi ina mkakati wa miaka minne na atahakikisha utekelezaji wa mkakati huo unaleta manufaa yaliyotarajiwa hasa kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya kuzalisha ajira, kuongeza kipato, kuboresha huduma za afya na utawala bora.
Balozi wa Uingereza Cancar amezungumzia kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi yake kuhusu kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, uchumi, na uwekezaji.
“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mhe. Rais Magufuli tunatazamia kukuza zaidi uhusiano wa Uingereza na Tanzania hasa katika biashara, kwa sasa biashara yetu ni takribani shilingi bilioni 390 kwa mwaka na pia tunachangia takribani shillingi bilioni 800 kwa mwaka katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapa Tanzania, matarajio yangu ni kuwa tutaongeza zaidi” alifafanua Cancar
Aliongeza kuwa uhusiano baina ya Tanzania na Uingereza ni mzuri na Taifa hilo ni moja ya washirika wakubwa wa maendeleo tangu uhuru ikiwa ni nchi ya pili kwa kuwa na miradi mingi Tanzania. Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Uingereza ina jumla ya miradi 927 Tanzania.
Miradi hiyo iko kwenye sekta mbalimbali na ina thamani ya Dola za Marekani milioni 5,390 na inatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 270,000, katika Sekta mbalimbali zikwemo elimu, utalii, mafuta na afya
Kwa upande wa Pakistani Balozi Mohamed Saleem amesema Tanzania ni nchi inayokuwa kiuchumi ikiwa na fursa nyingi za uwekezaji na kusisitiza kuwa utalii uko juu ambapo Pakistani itapanua wigo wake wa uwekezaji Tanzania
“Tanzania ni nchi nzuri, utalii uko juu, uwekezaji na uchumi unapaa na sisi tumeona kuna mambo mengi ya kushirikiana kwa siku zijazo, pia tutaongeza uwekezaji na ujenzi kwenye uchimbaji madini, viwanda na kilimo” alisema Saleem.
Kwa mujibu wa taarifa za TIC Pakistan ina jumla ya kampuni 100 zilizowekeza nchini zaidi ya Dola za Marekani 48,992 huku ikitoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 5,401.
Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali yake itatoa Amewaahidi Serikali itatoa ushirikiano wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwisho.