Maofisa ardhi wakitoa elimu ya kulipa kodi, nyumba kwa nyumba mtaa wa Ngarenaro Mjini Babati Mkoani Manyara.
Msajili wa hati msaidizi wa Mkoa wa Manyara, Elias Ndalichako akigawa kipeperushi kwa Mkazi wa Mjini Babati wakati akitoa elimu ya kulipa kodi ya ardhi.
………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Babati
KIKOSI kazi cha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi kimetua Mkoani Manyara na kuanza kutoa elimu ya ulipaji kodi ya jengo na ardhi, nyumba kwa nyumba ili kuisaidia Wizara kuuhisha taarifa zao na mifumo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi hilo mkuu wa kitengo cha kodi wizara ya Ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi Denis Masami alisema kuanza kwa zoezi hili ni ubunifu mpya wa kutembelea wamiliki wa nyumba na ardhi kwa lengo la kuwakumbusha kulipa kodi.
Aidha alisema zoezi hili ni endelevu na wanaendelea kulifanya ili kusaidia kuwajengea uwezo wamiliki wote wa ardhi na nyumba na kusaidia kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati ili kodi hiyo serikali iitumie kufanya mambo ya maendeleo.
Masami alisema wizara ya ardhi imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa mlipa kodi kila wiki siku ya ijumaa ambapo timu ya wataalamu wa wizara kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi wa mikoa na wilaya wanasambaa mitaani nchi nzima kutoa elimu nyumba kwa nyumba.
“Wajibu wetu sisi ni kutoa elimu namna ya kulipa kodi ya ardhi na unapopewa hati unapewa sharti la kumiliki ardhi ambalo ni kulipa kodi na wote wamiliki wa ardhi ni wapangaji,”alisema Masami.
Mtaalam huyo wa ardhi alisema kuanzishwa kwa zoezi hilo wananchi wanashukru sana huku akidai idadi ya walipa kodi imeongezeka.
Alisema baada ya mwezi mmoja sasa tayari wanakusanya sh. Bil. 10 kutokana na zoezi hilo kutoa hamasa.
Kaimu kamishna wa ardhi msaidizi mkoa wa Manyara, Leonard Msafiri alisema zoezi la kwenda nyumba kwa nyumba alilipokea vizuri na limekuja wakati mwafaka.
Msafiri alisema wananchi wengi wamebaini kumbe wanawajibu wa kulipa kodi na zoezi limeleta hamasa kwa watumishi kwa kuwa watumishi wanajifunza kutoka wizara na zoezi lina matunda sana.
Mkazi wa Negamsi Zuberi Njola akizungumzia zoezi hilo alisema litasaidia watu wengi na kupunguza urasimu kwa watumishi wasiowaaminifu kwa wateja.
Aliishauri Wizara kuwawezesha kikamilifu wataalamu wanaoendesha zoezi hilo nchi nzima.