Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam
Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa mazungumzo yao leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan kabla ya kuanza kwa mazungumzo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuonesha Balozi wa Canada nchini, Mhe. Pamela O’Donnell sheria ya uchaguzi kabla ya kumkabidhi sheria hiyo pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu masuala ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020
**********************************
Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza mahusiano ya kimkakati baina yao ili kuwezesha uwepo wa ulingo sawa miongoni mwa mataifa katika kusimamia maslahi na maendeleo ya nchi husika katika jumuiya za kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John kabudi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kusisitiza umuhimu wa Mataifa kuheshimiana na kutokubali kuingilia uhuru wa mambo ya ndani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu,demokrasia ama jambo lolote jingine.
Ameongeza kuwa mazungumzo hayo ya kimkakati yalilenga pia kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa 55 tangu Tanzania na China zisaini mkataba wa urafiki ambao uliweka msingi wa mahusiano makubwa na ya dhati katika nyanja za ulinzi na usalama,afya,kilimo, elimu na miundo mbinu ambapo mpaka sasa China ni Taifa linaloongoza hapa nchini kwa uwekezaji wa moja kwa moja kwa kuwekeza zaidi ya miradi 700 yenye thamani ya dola za Kimarekani (USD) bilioni 7.1 na kutengeneza zaidi ya ajira 87,000 kwa watanzania.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke amesema China wakati wote ni Rafiki mwaminifu na wa kudumu wa nyakati zote kwa Tanzania na kwamba kutimiza miaka 55 ya urafiki wa nchi hizo ni kielelezo tosha na siku zote wataendelea kuuheshimu na kuuenzi urafiki huo.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’Donnell, ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi na mabalozi waliadili masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mahusiano, uwekezaji na biashara, afya, elimu pamoja na utalii.