NA JOHN BUKUKU-DAR ES SALAAM
Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Humphrey Polepole amesema kwa mtu yeyote anayeamini mabadiliko makubwa aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk. John Pombe Magufuli katika jiji la Dar es salaam basi twende sote tukasimame naye pamoja kwenye mkutano mkubwa wa kampeni utakaofanyika kesho kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam ukijumuisha wana Dar es salaam wapenda maendeleo wote.
Polepole ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya Makao Mkuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam alipoutangazia umma kuhusu mkutano huo mkubwa wa kampeni wa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi CCM utakaojumuisha wasanii mbalimbali wa muziki hapa nchini.
Amesema kama kuna mtu yoyote mkazi wa Dar es salaam miaka mitano iliyopita alikuwepo anajua Makutano ya TAZARA, Ubungo, Barabara za Mtaani na maeneo mengine mengi yalikuwaje na sasa mabadiliko makubwa yametokea hana budi kusimama na Rais Dk. Magufuli kesho kwenye uwanja wa taifa.
Polepole ameongeza kuwa miradi mikubwa iliyofanyika Dar es Salaam kwa kiasi kikubwa ni maendeleo ya watu na vitu kwa pamoja haviwezi kukwepana kwa sababu ukifanya maendeleo ya vitu watu ndiyo wanaovitumia kwa hiyo ukifanya maendeleo ya vitu maana yake umefanya maendeleo ya watu.
Polepole amesema hivi karibuni Rais Dk. Magufuli alikuwa na ugeni wa kimataifa wa Rais wa Malawi, Komredi Lazarus Chakwera. Ni miongoni mwa shughuli za kujenga uhusiano wa kimataifa. Ubunifu wake umekuwa hamasa kwa marais wengine wa Afrika, wengine wanataka kuja kujifunza. Tumepokea marais kadhaa katika kipindi hiki cha kampeni hadi wengine tumewaomba waje wakati mwingine.”
Amebainisha kuwa ugeni wa Rais wa Malawi aliyekuwepo hapa nchini unajenga diplomasia ya kiuchumi.Tanzania kuwa nchi inayowezesha kusafirisha bidhaa kubwa kubwa kwenda Malawi kutokana na uwepo wa bandari ambazo zinapokea mizigo kutoka nje na kuzifikisha katika nchi zisizo na bahari ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundu, DRC na Malawi.
“Jana alikuwa eneo la Mbezi Luis na mgeni wake waliweka jiwe la msingi kituo cha mabasi cha kimataifa ambapo kuna ujenzi wa jengo kubwa lenye gorofa zaidi ya nane. Sasa tunaiona Dar es Salaam mpya. Baada ya kazi za ofisini ataendelea na kazi zake za kampeni.
Aidha, ameelezea mradi mkubwa wa kuboresha bandari ya Mtwara ambayo itakuwa na uwezo wa kupokea mzigo wenye ukubwa wa tani 400,000 ambapo mzigo huo utakwenda nchi mbalimbali za jirani. Vilevile kuna meli kubwa inayoweza kubeba tani 1000, ambapo treni yenye mabehewa zaidi ya 20 ndiyo itaweza kubeba mzigo huo.
Akizungumzia suala la wasanii kupamba kampeni za CCM, Polepole amesema hicho si kitu kipya kwa sababu hata kampeni za wapinzani wasanii wapo na hata katika mataifa makubwa wasanii wanatumiwa.
“Mwanasiasa gani asiyetumia wasanii, hata Barrack Obama alitumia Donald Trump na Putin wote katika kampeni zao wanatumia wasanii, kila mmoja anapenda muziki. Kesho tutakuwa na wasanii wakubwa katika kusherehekea mafanikio ya miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. Magufuli ndiyo maana hatuwaachi wasanii kwa kuwa sisi mbali ya kufanya kampeni lakini pia tunasherehekea mafanikio,” amesema.
Amewataja wasanii watakaokuwepo kwenye mkutano huo kesho kuwa ni Naseeb Abdul “Diamondplatnamz”, Ali Kiba “King Kiba” Harmonizer na wengine wengi watakaopamba mkutano huo mkubwa katika uwanja wa Taifa.