……………………………………………………..
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Ndugu Kheri Denice James amewataka wananchi wa kata ya Bugogwa kukiamini chama chake na kuchagua wagombea wa chama hicho kwa ngazi ya Uraisi, Ubunge na Udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 28, kwa kuwa wanazitambua changamoto za wananchi, wana uwezo wa kuzitatua na wanapoahidi wana uwezo wa kutekeleza.
Ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa kata ya Bugogwa katika viwanja vya Kabangaja ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya kampeni ya mgombea wa ubunge wa jimbo la Ilemela kupitia CCM Dkt Angeline Mabula ambapo amesema kuwa mwaka 2015 chama hicho kupitia wagombea wake wakiongozwa na Mhe Dkt John Magufuli waliahidi kuimarisha sekta ya elimu, afya, miundombinu, kilimo, biashara, mikopo na uwezeshaji wananchi kiuchumi jambo ambalo limetekelezwa zaidi ya ilivyodhaniwa
‘.. Nilikuwa mwenyekiti wa vijana wa wilaya hii, Nakumbuka tuliwaambia mkimchagua Magufuli mtayaona mambo, mkimchagua Angeline mtayaona mambo, Na tukayataja mambo yenyewe, tulisema tutajenga barabara, tutaleta maji, tutaleta umeme nakadharika, leo hii mmeyaona, hamjayaona?, Alisema
Kwa upande wake mgombea wa ubunge CCM jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula mbali na kuwashukuru wananchi hao kwa kuwachagua katika awamu iliyopita, Akawataka kuendelea kuwaamini tena kwa kipindi kijacho ili utekelezaji wa shughuli za maendeleo uweze kuendelea huku akibainisha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika eneno hilo ikiwemo umeme, maji, ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, ujenzi wa miundombinu ya barabara, mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sambamba na kuwawezesha wananchi kiuchumi
Nae katibu wa CCM mkoa wa Mwanza Ndugu Julius Peter akawaasa wananchi hao kutojaribu kuchagua wagombea kutoka vyama pinzani kwani ni watu wasiokuwa na agenda na kufanya hivyo ni kujicheleweshea maendeleo
Mkutano huo wa kampeni ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge mteule wa kundi la vijana kutoka Mkoa wa Simiyu Bi Lucy John Sabu, Mwenyekiti wa Uvccm Mkoa Mwanza na wajumbe wake wa kamati ya utekelezaji, mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela na wajumbe wake wa kamati ya siasa.