Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (katikati) akizungumza na wakufunzi wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Bihawana Dodoma jana alipotembelea kukagua utendaji kazi na kuagiza kibuni miradi ya kujitegemea kimapato.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akitazama bomba la maji wakati alipokagua utendaji kazi wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Bihawana mkoani Dodoma jana. Katibu Mkuu amekipa kituo hicho shilingi Milioni 10 ili kianzishe miradi ya kujitegemea na kupunguza utegemezi wa fedha za serikali.
………………………………………………………
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amewaambia Watumishi wa Idara ya Mafunzo Utafiti na Huduma za Ugani kuwa ziara ambazo amekuwa akifanya kwenye Vyuo Vya Mafunzo ya Kilimo (MATI’s) pamoja na Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (FTC) zina lengo la kujenga dhana ya kujitegemea ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa Watumishi na Wakulima nchini.
Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea Kituo cha Wakulima cha Bihawana, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Kusaya amesema tangu ateuliwe na Mhe. Rais Magufuli kuiongoza Wizara ya Kilimo; ametembelea Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI’s) vya Umma na Binafsi 14 pamoja na Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (FTC) vine (4) huku akiwa amebakiza Kituo kimoja tu na
kuongeza kote huko alipopita si kwa lengo la kufanya utalii bali kujenga dhana ya kujitegemea kiuchumi na wakati huo huo kujileteamapinduzi ya kweli ya kiuchumi.
Kusaya amewaasa Viongozi wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Bihawana kuwa wanapaswa kuongeza maeneo makubwa kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa na ya kimkakati hata kama yatakuwa nje au mbali ya Vituo vya Wakulima ili siku moja wazalishe mbegu bora au mazao ambayo; yatauzwa na kuleta faida kwa Vituo.
“Napenda kuwaona mkiwa mmeanzisha miradi mingi, muwe na mashamba
darasa ili mazao hayo yaje kuuzwa na fedha hizo zitumike kuendesha shughuli za usimamizi na maendeleo”.
“Napenda pia mfikirie kuongeza maeneo kwa ajili ya kuwekeza na muwe mkiongea na Viongozi wa vijiji au mitaa; kuwaomba maeneo makubwa kwa ajili ya kuongeza tija na faida katika kilimo”. Amekaririwa Kusaya.
Katika ziara yake hiyo; Katibu Mkuu Kusaya alitoa ng’ombe wakubwa wawili, vifaranga vya kuku 1,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa ufugaji pamoja na kutoa kiasi cha fedha cha shilingi milioni kumi (10,000,000) kama sehemu ya mtaji wa kuanzisha miradi ya kujenga dhana ya kujitegemea na kujiendesha kwa faida.
Sambamba na vitu hivyo Katibu Mkuu Kusaya pia alimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima cha Bihawana Emmanuel Mtenga pikipiki moja kwa ajili ya kuongeza ufanisi kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku.