************************************
Na Woinde Shizza, Arusha
Sakata la mlinzi wa Bilionea, Saniniu Laizer ,Manase William (48) mkazi wa Ilkiding’a wilayani Arumeru,aliyeuawa kikatili na watu wasiojulikana akiwa kazini katika mgodi wa madini ya Tanzanite Mererani limechukua sura mpya baada ya ndugu wa marehemu kuwatimua wawakilishi wa Bilionea Laizer katika kikao cha mazishi wakidai wameshindwa kutoa ushirikiano wa kifo cha ndugu yao .
Wakiongea katika kikao hicho kilichoketi nyumbani kwa marehemu jana, ndugu wa marehemu walidai kwamba hatua ya mmiliki wa mgodi huo,Saniniu Laizer kushindwa kufika nyumbani kwa marehemu tangu tukio hilo limetokea ni kuonyesha dharau kubwa kwa jamii yao ya wamasai na hawahitaji msaada wao katika mazishi ya ndugu yao.
Mwenyekiti wa kikao cha familia ambaye pia ni mzee wa ukoo, Godson Osing’a alisema kuwa hakuna haja ya kumbembeleza mmiliki wa mgodi katika kuja katika msiba wa ndugu yao nanfamilia imetangaza kutoshitikiana na wao kuwa tangu awali wameshindwa kutoa ushirikiano japo siku ya tukio Laizer ndio alikuwa wa kwanza kufika kwenye tukio akiwa na polisi.
“Jana (juzi)tulikubaliana kwamba Laizer atafika kwenye kikao cha leo ili kulia na wafiwa lakini badala yake ameshindwa kufika na kuwatuma wawakilishi ambao tuliwakataa hii ni dharau kubwa kwa hiyo sisi hatuwahitaji nendeni tutazika wenyewe” alisema Osinga
Wazee hao wa mila(Laigwanani) katika boma hilo la Marehemu walidai kwamba upande wa Laizer umeshindwa kuguswa na msiba huo kwani badala ya kuonyesha hisia zao katika tukio hilo baya la mauaji badala yake wanataka kuchangia mazishi jambo ambalo walidao hawahitaji msaada wao na watazika kwa gharama zao.
Akiongelea baada ya kutimuliwa katika kikao hicho mdogo wa Bilionea Laizer, Yako Laizer ,ambaye alimwakilisha kaka yake alisema kuwa wamesikitishwa na hatua ya ndugu wa marehemu kutupa ushirikiano katika.jambo hilo kwani hata wao wameumizwa ila kaka yake ameshindwa kufika katika msiba huo kwa sababu yupo safarini
Naye meneja wa mgodi huo ,Kiria Laizer alisema kuwa hatua ya wao kutimuliwa katika kikao hicho cha ndugu wa marehemu kimewasikitisha sana ila wanajipanga kuhudhulia mazishi ya marehemu na kwamba haki na stahiki za marehemu zitapatikana.
“Sisi kama sehemu ya familia hatuwezi kujilazimisha mahala ambapo hatupewi ushirikiano ila tutahakikisha haki na stahiki za marehemu zitapatikana na tumeiachia serikali kupata ukweli wa tukio hilo” alisema Meneja mgodi.
Marehemu Manase alikutwa ameuawa katika lindo lake alfariji ,septemba 27mwaka huu na mwili wake kufanyiwa uchunguzi katika hospital ya Mkoa Mt Meru Oktoba 3 mwaka huu na marehemu atazikwa nyumbani kwao katika makaburi ya familia siku ya jumamosi Oktoba 10 mwaka huu .