Home Mchanganyiko Rais wa Malawi kutembelea Tanzania kwa ziara ya siku tatu

Rais wa Malawi kutembelea Tanzania kwa ziara ya siku tatu

0

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Paramamgamba Kabudi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Jijini Dar es Salaam,  kuhusu ujio wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus Chakwera ambaye atakuwepo nchini kwa siku tatu.Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Paramamgamba Kabudi akizungumza na Waandishi wa Habari (Pichani) Jijini Dar es Salaam,  kuhusu ujio wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus Chakwera ambaye atakuwepo nchini kwa siku tatu, kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mamabo ya Nje.Balozi Kanali Wilbert Ibuge, kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbasi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbubakar Kunenge. 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubbakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Jijini Dar es Salaam,  kuhusu ujio wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus Chakwera ambaye atakuwepo nchini kwa siku tatu.

*******************************************

Na.Beatrice Sanga-Sanga.

Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus McCarthy Chakwera anatarajia kutembelea nchini Tanzania ambapo atafanya ziara ya Kitaifa ya  siku tatu, kuanzia tarehe 7 mpaka 9 Octoba, 2020, yenye lengo la kuimarisha uhusiano,  ushirikiano  na kuendelea kudumisha ujirani uliopo baina ya nchi hizi mbili

Mheshimiwa  Dkt Lazarus McCarthy  Chakwera atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Chakwera atatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali na uboreshaji wa miundombinu ya bandari hiyo lakini pia atatembelea kituo cha kuhifadhia mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center) ambacho kimekuwa alama muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi.

Dkt Chakwera akiwa na mwenyeji wake, Mhe. Rais John Pombe Magufuli  wataweka jiwe la msingi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi Mwisho ambapo hatua hiyo ni ishara ya ushirikiano na umoja katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari Mhe.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema uhusiano kati ya Tanzania na Malawi ni wa muda mrefu na unaendelea kuimarika siku hadi siku ambapo Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika nyanja za kisisasa, ulinzi na usalama, kiuchumi,  kijamii na yale ya kikanda hususan ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ( SADC) na Umoja wa Afrika.

“ Nchi hizi mbili sio majirani tuu, lakini watu wanaoishi Tanzania na Malawi ni ndugu na ni watu wa jamii moja. Hivyo tutakuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Malawi kuanzia kesho” amesema Prof. Kabudi.

Aidha Prof.. Kabudi ameongeza kuwa nchi ya Malawi ni kati ya nchi zenye uwekezaji hapa nchini ambao umejikita katika sekta mbalimbali zikiwemo fedha, uzalishaji, usafirishaji, ujenzi, kilimo pamoja na mafuta

Akizungumza  katika mkutano huo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge  amewataka wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wawe tayari kwa ajili ya ugeni huu mkubwa na wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kumpokea Rais huyo wa Malawi

Hii inakuwa ni ziara rasmi ya kitaifa  ya kwanza kwa Mhe. Rais Dkt Chakwera tangu aingie madarakani mwezi Juni, 2020. Kabla ya hapo, Dkt. Chakwera alifanya ziara za kikazi za siku moja moja katika nchi za Zambia na Zimbabwe.