Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Mhe. Julius Mtatiro akieleza jambo wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw.Charles Malunde (hayupo pichani) alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Wilaya wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Ushirika kwa msimu mpya wa Korosho 2020/21
Naibu Mrajis Bw. Charles Malunde alifafanua jambo la Ushirika alipokuwa Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya Tunduru Mkoani Ruvuma
Ujumbe wa Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (kushoto) na Wataalamu kutoka Taasisi za Kifedha (kulia) wakiwa katika kikao cha pamoja Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Julius Mtatiro Mkoani Ruvuma
Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Bumi Masubo akieleza jambo wakati wa kikao cha Maafisa Ushirika, Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika pamoja na Vyama vya Msingi (hawapo pichani)
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde (Kulia) akioneshwa sehemu ya Mazao yaliyohifadhiwa katika Ghala la Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru na Meneja wa Chama hicho Bw. Imani Kalembo (kushoto) hivi karibuni, Mkoani Ruvuma
…………………………………………………………………………………….
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mhe. Julius Mtatiro amesema Wilaya hiyo tayari ipo katika hatua za awali za mpango wa utekelezaji wa mradi wa kuanzisha mashamba ya Pamoja (Block farming) ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kasi ya Maendeleo kwa Taasisi na Vyama vya Ushirika.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufuatilia maandalizi ya Msimu mpya wa Korosho katika masuala ya Ushirika. Pamoja na kutathmni msimu uliopita ili kupata namna bora ya kuondokana na changamoto zilizojitokeza kwenye Vyama vya Ushirika kwa maboresho zaidi ya msimu mpya 2020/21.
Mhe. Mtatiro alieleza kuwa Wilaya hiyo iko katika utekelezaji wa mradi wa Mashamba ya Pamoja miongoni mwa miradi mbalimbali wilayani hapo. Akifafanua kuwa mradi huo unalenga kuongeza kiwango cha mazao ya Kimkakati yanayozalishwa Wilayani hapo kikilenga kuongeza uzalishaji wa zao la Ufuta pamoja na Korosho. Aliongeza kwamba mradi huo katika hatua za awali unatarajia kuhusisha Taasisi, Shule pamoja na Vyama vya Ushirika.
Akiunga mkono hatua hiyo Naibu Mrajis Malunde amepongeza jitihada zinazoendelea Wilayani hapo na kuahidi kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa timu ya Wataalamu watakaohitaji kushirikiana na Tume ili kufikia malengo hayo.
“Tume iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo taasisi za Fedha, mabenki na Taasisi mbalimbali zenye malengo ya kuendeleza na kuimarisha nguvu ya Ushirika kwa maendeleo ya Uchumi wa nchi yetu,” alisema Naibu Mrajis
Aidha, katika ziara hiyo Naibu Mrajis amewataka Maafisa Ushirika, Wajumbe wa Bodi wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) pamoja na Vyama vya Msingi Wilayani kuendeleza ushirikiano wa pamoja katika kazi zao. Akisisitiza utendaji wenye kuzingatia maadili, Sheria, Kanuni na Taratibu za Ushirika ili kuondokana na changamoto za malalamiko ya ubadhirifu ambazo zimekuwa zikijitokeza hususani katika misimu ya mazao.
katika kikao cha tathmini za kiutendaji wa Ushirika na Mrajis amewasisitiza Maafisa Ushirika kusimamia na kuratibu wakulima kufanya uhakiki wa taarifa zao za Benki mapema kabla ya kipindi cha malipo ili kuondoa dosari zinzoweza kuwepo na kutoa ufumbuzi mapema.
“Hakikisheni mnashirikiana na Mabenki kuhakiki taarifa za Akaunti za Wakulima, hii ikiwa ni pamoja na usahihi wa majina, namba za Akaunti, vitambulisho husika na masuala mengine ili wakati wa malipo ukifika pasiwepo na kasoro ya kumchelewesha mkulima kupata malipo,” alisisitiza Naibu Mrajis
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Bw. Hashim Mbalabala amesema maandalizi ya msimu yanaenda vizuri akitaja baadhi ya maandalizi hayo ni pamoja na uagizaji pamoja na usambazaji wa magunia katika Vyama vya Msingi. Akiongeza kuwa Chama hicho tayari kimeshaanza taratibu za awali za ununuziwa vipimo vya unyevu wa Korosho ili kuhakikisha Korosho inayokusanywa kwenye Vyama na kufikishwa maghalani inakuwa katika ubora stahiki kwaajili ya kupata bei na masoko nzuri yenye faida kwa wakulima.