……………………………………………………………………..
KIPAJI ni mtaji, kitunze sana, ipo siku kitakutoa! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kijana Patric Ntambula mkazi wa Nyakarilo, Halmashauri ya Buchosa kumfanyia sapraizi kwa kumkabidhi picha aliyomchora mgombea ubunge Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nyakarilo.
Akizungumza wakati akimkabidhi picha hiyo Shigongo, kijana Patrick amesema hakuwahi kupenda siasa lakini baada ya Shigongo kuteuliwa kuwania ubunge, alijikuta anapenda siasa kutokana na kuteuliwa kwake, kwani ni mtu ambaye anamwamini katika utendaji wake na anampenda sana na kuongeza kuwa anamuombea apate nafasi hiyo ya kuliongoza Jimbo la Buchosa kwani sababu atakuwa mkombozi wa vijana na wananchi wa Buchosa.
Aidha, Patrick ameomba endapo Shigongo atachaguliwa, basi akawasaidie vijana kupata mikopo ili waweze kukuza biashara zao pamoja na vipaji kama kipaji chake cha kuchora na vipaji vingine walivyokuwa nao vijana wa Buchosa.
Shigongo anaendelea na kampeni zake Jimboni Buchosa akinadi sera za chama chake cha CCM pamoja kumuomba ridhaa kwa wananchi ili wawachague viongozi wa CCM kuanzia kiti cha urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.